Kangi Lugola Kapiga Biti Zito Gereza Lolote Litakaloruhusu Simu na Madawa Kuingizwa Kwa Wafungwa

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema gereza litakalobainika kuingiza vitu visivyoruhusiwa ikiwamo simu, mkuu wa gereza hilo atakamatwa na kuwekwa ndani.

Lugola ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Julai 11, 2018 wakati alipotembelea gereza la Ukonga na kuzungumza na maofisa na askari wa jeshi hilo.

Amesema matukio ya uingizaji wa simu na dawa yamekithiri katika magereza mbalimbali likiwamo la Ukonga na kwamba hatakubali kuona suala hilo likiendelea.

"Tutamweka ndani mkuu wa gereza husika na wale askari walioko zamu wakati vitu hivyo vinaingia watakuwa katika wakati mgumu sana.Watapata misukosuko,"amesema Lugola.

Lugola ambaye pia ni askari polisi mstaafu amesema haingii akilini wafungwa kufanya mawasiliano wakiwa gerezani.

Amesema wafungwa hao wamekuwa wakishirikiana na askari wasiowaaminifu katika mchakato huo wa mawasiliano.

“Sitakubali hali hii iendelee nitakuwa mkali sana.Kabla sijatumbuliwa na rais nitahakikisha wewe wa chini yangu utumbo uko nje ili nipate cha kujitetea, nataka kila abiria abebe mzigo wake,"amesema Lugola.

Ameongeza kuwa Rais John Magufuli amechoshwa kusikia taarifa za uingizaji wa vitu visivyoruhusiwa hasa simu kwenye magereza.

Awali akimkaribisha Lugola Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa alimpongeza waziri huyo kwa uteuzi na kuahidi kuwa jeshi hilo lipo litampa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad