Klabu ya soka ya Yanga imefanya mabadiliko kadhaa kwenye uongozi wake katika ngazi mbalimbali huku miongoni mwa waliopata nafasi ni nahodha na mchezaji mkongwe Nadir Haroub 'Canavaro' akiteuliwa kuwa meneja wa timu.
Mabadiliko hayo yametangazwa na Yanga kwenye kikao na wahahabari kiichofanyika mchana wa leo Julai 28, 2018, makao makuu ya klabu ambapo mkongwe huyo aliyewahi kunukuliwa na kipindi cha KIKAANGONI cha East Africa Television akisema kuwa lengo lake ni kuja kuwa kiongozi wa soka, sasa amepata fursa hiyo.
Baada ya kutangazwa, www.eatv.tv imemtafuta Nadir Haroub ili kujua atatumikiaje nafasi hizo mbili ya nahodha na meneja, lakini ameeleza kwa kifupi kuwa amepokea taarifa hizo bila kuwepo kutokana na kuwa nyumbaji kwao Zanzibar akimuunguza mama yake ambaye anaumwa.
''Nimechaguliwa kuwa meneja kweli nimesikia ila siwezi kusema chochote nipo namuuguza mama yangu na hayupo kwenye hali nzuri naomba tuongee baadae nitaeleza mapokeo yangu'', - Nadir.
Nadir anachukua nafasi ya Hafidh Saleh ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo na sasa ameteuliwa kuwa mratibu wa timu. Yanga kwasasa inajiandaa na mchezo wake wa marudiano wa kombe la shirikisho barani Africa dhidi ya Gor Mahia. Mchezo huo utapigwa Jumamosi kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.