Kesi inayomkabili Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando imepigwa tena kalenda na itasikilizwa Julai 18 mwaka huu.
Kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa leo Julai 12, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Leonard Swai alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa shahidi waliyemtarajia atoe ushahidi leo ana udhuru hivyo akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi aliipanga kesi hiyo hadi Julai 18,2018 ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi katika kesi hiyo, ambao ni Ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.
Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Tido anatetewa na Wakili Ramadhani Maleta na yupo nje kwa dhamana.