YANGA wameendeleza mwendo ambao siyo mzuri katika michuano ya kimataifa baada ya kuruhusu kupata kichapo kutoka kwa Gor Mahia cha mabao 3-2 kwenye mchezo wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga wameshacheza michezo minne hadi sasa kwenye Kundi D ambalo lina timu nyingine ambazo ni USM Algers ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda, lakini hawajapata ushindi kwenye mchezo hata mmoja.
Matokeo ya mchezo wa jana yanamaanisha kuwa sasa Yanga wamebakiza michezo miwili tu kwenye kundi lao na hawana matumaini ya kufuzu. Katika michezo miwili ambayo Yanga wamekutana na Gor Mahia hivi karibuni, wamefungwa jumla ya mabao saba, baada ya mchezo wa kwanza kufungwa 4-0 jijini Nairobi.
Katika mchezo wa jana, kipa wa Yanga, Youth Rostand alifanya makosa kadhaa ambayo yalichangia mabao mawili ya mwanzo ya Gor Mahia.
Rostand alifanya kosa katika sekunde ya 35 tangu kuanzia kwa mchezo hu ambapo aliucheza mpira vibaya uliopigwa kichwa na George Ogutu na kujaa wavuni.
Hata hivyo, aliendelea kufanya makosa ya mara kwa mara ambapo dakika ya 41 kipa huyo aliudaka mpira akaurusha vibaya kabla haujaguswa na mchezaji mwingine akaudaka tena, mwamuzi akaamuru kuwa ni faulo ambapo Jacques Tuisenge aliifungia timu hiyo bao la pili.
Dakika ya 55, Deus Kaseke, ambaye alicheza mchezo wake wa kwanza tangu asajiliwe na Yanga, hivi karibuni aliifungia timu yake bao moja baada ya kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch kuutema mpira.
Hata hivyo, matumaini ya Yanga hayakudumu kwani dakika ya 64, Gor Mahia walifunga bao la tatu kupitia kwa Haron Shakava baada ya mabeki wa Yanga kufanya uzembe. Dakika ya 75, Yanga walimtoa Rostand na nafasi yake kuchukuliwa Beno Kakolanya ambapo wakati anatoka mashabiki walikuwa wakimzomea.
Dakika tano baadaye Raphael Daudi aliifungia timu hiyo bao la pili baada ya kipa kushindwa kukoa shuti lililopigwa na Ibrahim Ajibu. Hata hivyo, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera hakuonekana kwenye mchezo huo ambapo Noel Mwandila ndiye alikuwa anatoa maelekezo kwenye benchi.
Kidomo Domo Chawaponza Yanga Wachapwa Tena Kipigo cha Mbwa Mwizi na Gor Mahia
0
July 30, 2018
Tags