Kigwangalla Atoa Siku 90 Kufanyika kwa Sensa ya Mamba

Kigwangalla Atoa Siku 90 Kufanyika kwa Sensa ya Mamba
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk.  Hamisi Kigwangalla, ametoa miezi mitatu kwa Taasisi ya utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kufanya utafiti na sensa ya mamba katika ziwa Rukwa ili kubaini idadi yake.

Alisema baada ya utafiti huo ataishauri serikali namna ya kudhibiti madhara yanayosababishwa na mamba hao kwa wananchi hususan wa jimbo la Songwe, ikiwamo kuwavuna kama idadi yao itabainika kuwa kubwa.

Dk. Kigwangalla alitoa agizo hilo jana katika kijiji cha Maleza Kata ya Mbangala Wilaya ya Songwe mkoani Songwe alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kutatua mgogoro uliopo baina ya wananchi na mamba wa Ziwa Rukwa.

“Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori ambayo ipo chini ya wizara yangu, nawaagiza wafike hapa mara moja na ndani ya miezi mitatu wanipe majibu nini kifanyike kupunguza madhara yanayotokana na mamba kwenye Ziwa Rukwa, wafanye sensa watuambie kuna mamba wangapi, lakini pia watushauri nini tufanye ili kudhibiti mamba hao wasiendelee kusababisha athari kubwa kwenye maisha ya watu wanaoishi jirani, lakini pia wanaoutumia ziwa.

“Kwa sababu madhara yanaweza yakawa mengi, inawezekana mamba wameshakuwa wengi na samaki wamebaki wachache, hivyo hata mamba nao mwishowe wataanza kufa ama wataanza kutafuta chanzo kingine cha chakula pengine ndio maana wameanza kutafuta binadamu anayekwenda ziwani kwa sababu sasa wanakuwa na njaa, inabidi wasogee ufukweni wawinde chochote kinachosogea karibu na maji,” alifafanua Dk. Kigwangalla.

Dk. Kigwangalla alitoa agizo hilo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo, ambaye alisema kumekuwapo na matukio mengi ya mamba kushambulia na kuua wananchi wa vijiji jirani wanaofuata huduma mwambao wa Ziwa Rukwa.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuandaa mpango wa kitaifa kwa kila wilaya na vijiji nchini utakaoweka utaratibu maalum wa namna na sehemu wananchi watakayopata huduma ya kuni na mkaa.

“Utaratibu uwekwe na muuweke nchi nzima, kila wilaya, kila kata, kila kijiji uwekwe utaratibu wananchi watapata wapi mkaa, watapata wapi kuni, kibali cha kuvuna kitapatikana wapi, utaratibu uwe wazi, sio kusubiri kwenye mageti unakamata, hapana weka utaratibu kwanza, ukishaweka utaratibu atakayevunja sheria hata ukimkamata ukimpeleka polisi utakuwa umemrahisishia OCD kazi,” alisema.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad