Kijana Ngassa Mathias (24), mkazi wa Kitongoji cha Kiloleli, Kijiji cha Ilebelebe, Kata ya Itilima, Wilaya ya Kishapu amekamatwa na jeshi la polisi baada ya mama yake mzazi, Nyawamba Dohoi kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya kichwani na mikononi na watu wasiojulikana.
Kutokea kwa mauaji hayo na kukamatwa kwa kijana huyo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Simon Haule. Akizungumza na mwandishi wa Uwazi kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilebelebe, Thomas Nkindo alisema kuwa inashangaza mauaji hayo yanayolenga wanawake kutokea, kwani mwaka jana mwezi kama huu kulitokea mauaji ya mwanamke mmoja aliyeuawa kikatili kama huyu.
Nkindo alisema kuwa wananchi wengi wamekimbia kijiji baada kutokea mauaji ya marehemu Nyawamba yaliyofanywa na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika.
“Nitaitisha mkutano wa hadhara wa wananchi ili kubaini tatizo hili kwani msiba huu ni mkubwa, watu wasiwe wanaingia kijijini kwetu kufanya mauaji ya kinyama, hatuwezi kusema marehemu alikuwa na ugomvi na nani bali tuangalie ni akina nani waliotenda haya. “Kutokana na mauaji haya, watu wanaogopa kuja msibani kwa hofu na wengine wamekimbia kijiji kwa hofu ya kukamatwa na polisi,” alisema mwenyekiti huyo wa kijiji.
Wifi wa marehemu, Sia Shija alisema kuwa waligundua kuuawa kwa marehemu saa tatu asubuhi baada ya jirani mmoja kwenda nyumbani kwake kuchukua ndoo yake aliyokuwa ameiazima marehemu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Simon Haule amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mwishoni mwa wiki iliyopita huku akieleza kuwa mauaji hayo chanzo chake ni ni mali alizoachiwa marehemu na mume wake ambaye naye ni marehemu. “Hivi sasa tunamshikilia mtoto wa marehemu, Ngassa Mathias kwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo,” alisema Kamanda Haule.