Kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa ya Zimbabwe ya mchezo wa Rugby wamelazimika kulala mtaani wiki hii nchini Tunisia baada ya kulalamikia huduma duni waliyopata kwenye hoteli waliyoandaliwa.
Picha kadhaa zimepostiwa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana hao wa Zimbabwe wakiwa wamelala kandokando mwa kituo cha mabasi nchini Tunisia wakati wakiwa kwenye maandalizi ya mchezo wao wa kufuzu michuano ya kombe la dunia dhidi ya wenyeji utakao pigwa Jumamosi ya wiki hii.
Mbali na kulala mtaani usiku wa vijana hao pia ulikuwa mmbaya baada ya kucheleweshwa kwenye uwanja wa ndege kwa saa sita nyakati za usiku kutokana na kucheleweshewa taratibu za Viza.
Baada ya Zimbabwe kuandika barua rasmi ya kulalamikia kitendo hicho mara tu walipofika kwenye hoteli hiy Shirikisho la Mchezo wa Rugby nchini Tunisia limeshtumu nchi hiyo kwa kitendo chake cha kuchua maamuzi ya kwenda kulala kwenye mitaa bila hata kuangalia uhusiano wa nchi hizo mbili.
Shirikisho la Mchezo wa Rugby Barani Africa limeomba radhi kwa jambo hilo lililotokea na kuwapangia hoteli nyingine.
Timu hiyo ya taifa ya Zimbabwe ambayo inashika nafasi ya nne ipo nchini Tunisia ambao ndiyo wandaaji wa mashindano hayo wakitafuta tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la dunia.