Julai 12 2018 Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilipitisha kanuni za kuruhusu usajili wa idadi ya wachezaji 10 wa kigeni katika Ligi Kuu kuanzia msimu ujao watakaoweza kutumika wote kwa wakati mmoja.
Kutokana na maamuzi hayo, mashabiki wengi wa Yanga wamepingana na maamuzi hayo na hii ni kutokana na klabu yao kuyumba kifedha kipindi hiki.
Mashabiki hao wengi wameonekana kuandika mitandaoni wakilalamika juu ya suala hilo wakiamini timu yao haiwezi kusajili wachezaji wazuri wa kimataifa kutokana viongozi wa timu yao kukabiliwa na uhaba fedha.
Lakini wale baadhi wa upande wa pili ambao ni Simba wameonekana kuchekelea kutokana na timu yao kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji, na kumkabidhi tajiri kijana na bilionea, Mohammed Dewji, wakiamini klabu itasajili mchezaji yoyote yule kwa sasa.
Ukiachana na mitandaoni, katika vijiwe vya maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam baadhi yao wamekuwa wakipinga huku wengine wakisifia wakiamini italeta ushindani mkubwa.
Walioamini ushindani utakuwepo wameeleza ni kutokana na wazawa watapaswa kujituma zaidi Uwanjani ili kujiwekea namba kwa lengo la kushindana kiuwezo na wageni, hivyo itakuwa ni changamoto kwao kujipanga zaidi ili kufanya vizuri.