Kimenuka..Lugola Amvaa Kamanda Sirro, Ampa Wiki Mbili


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amempa wiki mbili Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, amweleze kama Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro.

Lugola alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akiwa katika ziara ya kikazi Makao Makuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kilichopo Ukonga ambako pia aliongea na askari wa kikosi hicho.

“Ninamwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi ndani ya wiki mbili afike ofisini kwangu na timu ya makamishna alionao Makao Makuu ya Polisi, aniambie huu uchumi wa kati ambao Rais amelenga tuufikie, mahusiano yake na Jeshi la Polisi:

“Aniambie Watanzania tunataka wafanye shughuli za kiuchumi saa 24, hatuwezi kufikia malengo ya uchumi wa kati kama Watanzania watafanya kazi saa 12 au nane,” alisema.

Alimtaka IGP pia amweleze iwapo hatua ya mabasi kutokutembea usiku imewashinda na kunyoosha mikono kwa majambazi.

“Biashara zinafungwa saa 12 jioni ukiuliza wanasema ni kwa sababu ya usalama, IGP aje aniambie Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi?” Alihoji.

Waziri Lugola aliongeza “Hatuwezi tukakubali kupewa amri na majambazi wakatupangia ni saa ngapi tufanye shughuli za kiuchumi au ni maeneo gani twende au tusiende,” alisisitiza.

Nipashe ilipomtafuta kwa njia ya simu IGP Sirro, kuhusu kupokea agizo hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad