KIONGOZI wa mbio za mwenge mwaka huu, Charles Kabeho ,amekataa kuzindua mradi wa upanuzi wa kituo cha afya cha Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.
Hali hiyo imezua sintofahamu mara baada ya kusomwa ripoti ya matumizi ya fedha ambazo hazijaeleweka zimetumikaje huku serikali ikiwa imechangia kiasi cha sh.milioni 400.
Aidha kwa mujibu wa taarifa ya wilaya imedaiwa wananchi wamechangia milioni tatu wakati taarifa ya mkoa inaonyesha ilichangia milioni moja.Akizungumza kwenye kituo hicho cha afya, Kabeho alishtushwa na kuhoji kutokea kwa hali hiyo.
Alimtaka mkuu wa wilaya atoe kauli yake na kukataa kuuzindua mradi mpaka watakapotoa taarifa ya uhakika.Kabeho aliasa halmashauri na wilaya mbalimbali ,kusimamia miradi ya maendeleo ili iendane na thamani halisi ya fedha .
Nae mkuu wa wilaya ya Rufiji,Juma Njwayo aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama hususani taasisi ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) kufuatilia suala hilo.Kati ya miradi tisa ambayo ilipaswa kukaguliwa,kuwekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa wilayani Rufiji ,iliyogharimu bilioni 2.654.40 mradi huo mmoja ulikwama kuzinduliwa .
July 13 mwenge huo ulikuwa Rufiji na July 14 umetembelea miradi ya maendeleo katika wilaya ya Kibiti.