Kiwanda Cha Sukari Kagera Chaagizwa Kuacha Urasimu

Kiwanda Cha Sukari Kagera Chaagizwa Kuacha Urasimu
Uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera umeagizwa kuacha urasimu katika mfumo wa uuzaji wa Sukari wanayozalisha badala yake kuingiza mtaani kwa wingi Sukari kwa wananchi ili kuepuka kadhia ya upungufu wa huduma hiyo muhimu katika jamii.

Agizo hilo limetolewa na Mawaziri wa sekta ya Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba na waziri wa sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage wakati wakizungumza na uongozi wa kiwanda hicho Jana 11 Julai 2018 walipotembela kiwanda cha Sukari wakiwa kwenye ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani humo iliyoanza Juzi 10 Julai 2018.

Mawaziri hao kwa kauli moja wametoa siku 14 kwa kiwanda hicho kuongeza kasi ya uzalishaji kutoka uzalishaji wa Sukari kwa Tani 350-360 kwa siku ili kufikia walau Tani 450 mpaka 500 kwa siku kwani kufanya hivyo wataimalisha uwezo wa Sukari kupatikana kwa wingi kwa wananchi hivyo kuondoa usumbufu wa gharama katika ununuzi wa bidhaa hiyo.

Aidha, Mawaziri hao wametoa kalipio Kali kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa na mawakala wachache wa usambazaji wa sukari jambo ambalo linapelekea ushindani wa kibiashara kuwa mchache mbinu inayopelekea Sukari kuuzwa kwa gharama isiyokuwa rafiki kwa watumiaji.

Walisema kuwa ndani ya muda mfupi uongozi wa kiwanda hicho unapaswa kutathmini upya namna ya kuongeza Uwekezaji ili kurahisisha huduma za wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 hatimaye kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025.

Dkt Tizeba alisema kuwa kumekuwa na uingizaji wa Sukari kwa magendo kutoka nje ya nchi kwa sababu Viwanda vya Sukari ndani ya nchi vimefungia sukari kwenye magodaoni bila kuingiza sokoni kwa wingi kuwafikia watumiaji.

Pia, alisema kuwa wataalamu wa kiwanda cha Sukari wanapaswa kutoa elimu ya muwa kwa umma ili kuona umuhimu wa uzalishaji wa zao hilo sambamba na kushirikiana na wakulima wadogo zaidi ya 490 katika vijiji vya jirani na kiwanda hicho.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage alisema kuwa serikali inatazama namna bora zaidi ya kukuza takwimu za uzalishaji wa Sukari nchini hivyo Viwanda vya Sukari vinapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchochea Uwekezaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Pia alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli haitasita kuvifungia Viwanda vyote vitakavyobainika kukiuka taratibu, sheria na kanuni za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad