Kocha wa timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse amepewa mkataba mpya kuendelea kuifundisha timu hiyo huku akipewa sharti zito kuelekea michuano ya mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini, Cameroon.
Katika mkataba huo mpya, Aliou Cisse amepewa sharti la kuifikisha timu hiyo katika fainali za michuano ya Afrika ili kujihakikishia nafasi ya kuendelea kwa miaka mingine.
Wakati wa hafla ya upokeaji wa taarifa ya kiwango cha timu hiyo katika michuano ya kombe la dunia iliyokwisha mwezi huu nchini Urusi kutoka kwa kocha, Rais wa shirikisho la soka la Senegal, Augustin Senghor amesema.
“Katika tathmini ya mkataba wake, tunaona amefikia mafanikio yake ya awali ya kuiwezesha timu kufuzu michuano ya kombe la dunia ambapo ulimwengu mzima umetambua kuwa alifanya juhudi za kuipeleka Senegal katika hatua kubwa “.
“Tunaona hakuna sababu ya kushindwa kuendelea naye, kwahiyo tumempangia kazi nyingine ya kuhakikisha anaifikisha fainali timu yetu katika michuano ya mataifa ya Afrika “. Ameongeza, Senghor.
Senegal iliweka rekodi kuwa timu ya kwanza kuondolewa katika hatua ya makundi ya kombe la dunia kwa sheria ya ‘Fair play’ baada ya kulingana kila kigezo na timu ya taifa ya Japan ambayo ilisonga mbele katika hatua ya 16 bora.
Aliou Cisse (42) alikuwa katika kikosi cha Senegal kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka 2002 nchini Japan ambacho kiliifunga bingwa mtetezi Ufaransa na kilifika hatua ya robo fainali. Aliteuliwa kuiongoza Senegal mwezi March, 2015 baada ya kuiongoza timu ya vijana ya nchi hiyo katika michuano ya Olympic nchini Uingereza mwaka 2012.