Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amedai aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba anapaswa kushtakiwa kwa kuwa ameshindwa kusimamia mambo mengi wakati akiwa waziri.
Nassari ametoa kauli hiyo leo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ikiwa zimepita saa kadhaa tangu kutangazwa kwa mabadiliko ya baraza la mawaziri, huku Mwigulu akiachwa.
“Kutumbuliwa kwa Mwigulu hakumsafishi kwa wananchi. Mengi ameshindwa kusimamia kwa maslahi yetu. Alikuwa wa kwanza kusema kuwa Abdul (Nondo-mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam) alijiteka,” amesema.
“Watu wamepotezwa wameokotwa kwenye viroba na (Mwigulu) kusema ni jambo la kawaida. Alitakiwa kushtakiwa kwa kugharimu maisha ya watu.”
Hata hivyo baadhi ya watu walichangia alichokieleza Nassari walimuunga mkono na wengine kupingana naye.
Mmoja wa watu hao, Miriam Shelutete amesema, “sioni kama kuna ovu lolote alilofanya linalongojea kupata msamaha wa wananchi, alisimamia alichokiamini na kutufikisha hapa tulipofika leo.”
“Uwaziri wake haikuwa dhamana ya milele, kwa wakati ule alionekana ni mtu sahihi ila kwa wakati huu amepatikana mwingine wa kuendeleza safari.”