Siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola, kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro kuhusu mbwa na ujambazi, jana amemtaka ampelekee orodha ya miaka mitano ya matukio ya utekaji wa bodaboda na kuuawa kwa madereva wake.
Waziri Lugola alitoa agizo hilo jana akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha katika Kituo cha Polisi cha Muriet.
Akiwa ziarani humo alipata fursa ya kusikiliza kero za wananchi ndipo waendesha bodaboda hao walipotoa malalamiko yao kuhusu kutekwa na kuuawa wakiwa kazini.
Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Kata ya Muriet iliyopo mjini humo, Akili Mbaga, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alimweleza Waziri Lugola kuwa, wamekuwa wakiuawa na wezi wa bodaboda na kesi zimejaa polisi bila kufuatiliwa.
Mbaga alimuomba Waziri Lugola awasaidie ili matukio hayo yakomeshwe.
Kutokana na ombi hilo, Waziri Lugola alisema anajua baadhi ya maeneo madereva wa bodaboda wamekuwa wakitekwa na wakati mwingine wakizuiliwa barabarani na magogo kisha kunyang’anywa vyombo vyao vya usafiri na kuuawa.
“Ninamwelekeza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) aniletee orodha ya miaka mitano iliyopita mpaka sasa ikiwa na takwimu kwa maeneo, kiwilaya na kimkoa na nchi kwa ujumla, niweze kuona matatizo haya yamekithiri hasa maeneo gani ili tuwe na mikakati ya kujipanga kwa kuongeza nguvu kuhakikisha matatizo haya yanamalizika,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya kumtaka IGP kumpelekea orodha hiyo, ina lengo la kutafuta mwarobaini wa kuyamaliza matukio hayo.