Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amepiga marufuku uwekaji wa alama ya ‘X’ kwenye makazi ya wananchi waliojenga katika maeneo ambayo hayajarasimishwa kote nchini.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wadau wa ardhi waliokutana kujadili mpango mji wa miaka 20 wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba yake kwa sababu amejenga katika eneo ambalo halijarasimishwa, kwa sababu Serikali imewapa fursa ya kurasimisha maeneo hayo.
Pia alizipiga marufuku kampuni zinazojihusisha na urasimishaji wa maeneo kuwachangisha fedha wananchi kutokana na kubaini kuwapo kwa kasoro kadhaa wakati wa zoezi hilo maeneo ya jijini Dar es Salaam.
“Zoezi hili tulilianza tukaona lina kasoro, Dar es Salaam kuna watu walianza kutoza wananchi Sh 500,000 hadi Sh 400,000 ili kupima kiwanja kimoja cha maskini aliyejenga kwenye eneo lisilo rasmi.
“Lakini baada ya kuchunguza nimegundua gharama halisi hazizidi Sh 250,000, kwa hiyo nimetoa agizo kwamba katika urasmishaji wowote hapa Tanzania, mwananchi asichangie zaidi ya Sh 250,000 ili kupimiwa kiwanja chake hiyo ni gharama ya juu.
“Kampuni hizi zishindane kwa sababu tenda zitatangazwa na wilaya ili kila mtu anayetaka kupata kazi lazima atoe bei isiyozidi Sh 250,000 na iwe marufuku kwa kampuni kuchangisha fedha za wananchi katika sehemu ambayo inarasimishwa.
“Dar es Salaam yako makampuni matatu yamechukua fedha, wananchi wamechangisha kwenye akaunti zao na wametoroka hawakufanya kazi, hawa tunawakamata.
Alisema wakati wa urasimishaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali wananchi wenyewe watafungua akaunti zao za mitaa ambazo watazisimamia.
Aliwaonya viongozi wa mitaa kujihusisha na fedha hizo na kwamba, malipo yatafanyika baada ya kazi hiyo kuthibitishwa na maofisa wa wilaya.
Alisema gharama zitakazotumika kurasimisha zitakapokubaliwa ndipo wananchi watatoa fedha kuzilipa kampuni zitakazopewa kazi hiyo.
“Najua watendaji na wapimaji wa Serikali ni wachache, ndiyo maana tumeweza kusajili kampuni nyingi za upimaji, kwa hiyo ni marufuku kwa kampuni binafsi kwenda kuomba kazi huko mitaani, lazima waanzie wilayani na isimamiwe na wilaya. Na iwe kiungo kati ya wale warasimishwaji na warasmishaji.
“Narudia, ni marufuku kwa kampuni kuchukua fedha za wananchi na kuingiza kwenye akaunti zao. Lakini iwe tena ni marufuku kwa madiwani na wenyeviti wa mitaa kwa sababu baadhi yao wamekuwa wanachukua fedha kwa makampuni wakidanganya kuwa wao ndio wanatoa kazi za urasimishaji na upimaji.
“Matokeo yake wanataka kuhongwa fedha na gharama hizo zinaingia kwenye gharama za watu wanaotaka kurasimishiwa. Kazi hazitatolewa na mwenyekiti wa mtaa wala diwani, zitatolewa wilayani kwa hiyo kampuni zisiende kwenye mitaa kuhonga madiwani au wenyeviti wa mitaa ili wapate kazi ya urasimishaji,” alisema.
Waziri Lukuvi aliwataka watendaji wote wa ardhi wa wilaya zote nchini kuhakikisha wanasimamia zoezi la urasimishwaji na uhamasishaji na kwamba, migogoro yoyote itakayotokea watawajibika.
“Isitokee mtu tena akaweka X kwenye nyumba za wananchi kama ilivyojitokeza Babati jana (juzi), katika maeneo ambayo watu wamejenga kiholela isipokuwa kwa watu waliojenga kwenye maeneo yaliyo kwenye hifadhi zilizopo kwa mujibu wa sheria, kama vile hifadhi ya barabara, hifadhi ya misitu iliyosajiliwa au iliyotangazwa kwenye gazeti la Serikali,” alisema Waziri Lukuvi.
Waziri Lukuvi alizitaka wilaya zote kuhakikisha zinaainisha maeneo yote ambayo hayajarasimishwa ili kupanga utaratibu wa zoezi hilo ili wananchi wapate barabara, hati miliki za maeneo hayo kulingana na nyumba walizozijenga.
“Barabara watazipata kwa kukubaliana wenyewe ni nani achangie ardhi yake ili barabara iweze kupita na kila mwananchi atachanga fedha kuhakikisha nyumba yake inapimwa kwa gharama zake,” alisema Lukuvi.