Mabasi Mwendokasi Kufanyiwa Mabadiliko ya Ratiba zake


Kampuni  inayotoa huduma kwenye mfumo wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (UDART), imesema kuanzia Julai 30 mabasi yanayoanza na kumaliza safari zake katika kituo cha Ubungo Maji yataishia Ubungo Terminal.


Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Deus Bugaywa, alisema mabadiliko hayo ni kutokana na shughuli za ujenzi wa daraja la juu kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma.


Alisema  wamelazimika kubadili ratiba ya mabasi hayo yaliyokuwa yakianzia na kumalizia safari zake katika kituo cha Ubungo Maji, huku yakitumia njia moja na nyingine kutumika na magari mengine.


Alisema wakati wa asubuhi mabasi yanayotoa huduma ya ‘Express’  njia  namba 002 kutoka Ubungo hadi Kivukoni na njia namba 005 kutoka Ubungo mpaka Gerezani yatalazimika kuanzia safari zake kituo cha Ubungo Terminal badala ya Ubungo Maji.


“Nyakati za mchana na jioni mabasi ya njia hizo yataendelea na huduma za kawaida zisizokuwa express na hatua hii itadumu kwa miezi  miwili hivyo tunawaomba radhi wateja wetu kwa usumbufu utakaojitokeza.


“Wakati wa shuguli za ujenzi wa barabara hizo mabasi ya mwendo wa haraka yatakuwa yakitumia njia moja tu, ndiyo maana mabasi yetu yataishia Ubungo Terminal  kupunguza msongamano wa mabasi kituoni wakati wa kushusha abiria,” alisema Bugaywa.


Alisema  kutokana na mabadiliko hayo,  aliwashauri abiria waliokuwa wakitumia kituo cha Ubungo Maji hasa nyakati za asubuhi kutumia zaidi kituo cha Ubungo Terminal au Kibo kuondoa usumbufu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad