Maelfu ya Vijana waliohitimu mafunzo ya JKT na Mgambo na hawana kazi jana walifurika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda kwaajili ya kupatiwa ajira ya kusimamia kikamilifu suala la usafi na kuwatoza faini wanaochafua mazingira.
Akizungumza na Vijana hao RC Makonda ametangaza Rasmi kutengua kipengele kilichokuwa kikiwataka Wafanyabiashara kufunga maduka yao siku ya Jumamosi hadi Saa nne asubuhi kwaajili ya usafi na badala yake amewakabidhi jukumu hilo vijana wa JKT na Mgambo ambapo watakuwa wakiwakamata wafanyabiashara watakaokaidi kufanya usafi.
Aidha RC Makonda amesema vijana hao watakuwa na jukumu la Kusimamia kampuni zilizopewa kazi ya Usafi kwenye maeneo husika, Kuwakamata, kuwatoza faini watupaji wa taka pamoja na kufuatilia kujua kila nyumba inapeleka wapi taka wanazozalisha ambapo ifikapo Jumanne ya Julai 10 itakuwa ndio mwisho wa usajili wa vijana hao.
Hata hivyo RC Makonda amewataka vijana hao kutotumia nguvu kuwaadhibi watu watakaotii Sheria huku akiwahimiza pia kuwakamata vibaka wanaopora Mali za watu.
Kabla ya vijana hao hawajaanza kazi watapatiwa mafunzo ya sheria ya mazingira ili waweze kutekeleza majukumu yao pasipo kumuonea mtu.