Magufuli Atoa Agizo Hili kwa Baraza la CCM

Magufuli Atoa Agizo Hili kwa Baraza la CCM
Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amelitaka Baraza la Wadhamini la chama hicho kuhakikisha CCM inanufaika na mali zake na kuachana na utegemezi wa kuomba misaada kutoka kwa watu.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Baraza hilo jipya ambao ni Anna Margareth Abdallah (Mwenyekiti), Ndg. John Zephania Chiligati, Jaji Mstaafu Mark Bomani, Balozi Mstaafu Daniel Ole Njoolay, Pandu Ameir Kificho, Christopher Gachuma, Dkt. Haruni Kondo na Hassan Omar Mzee, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

"Katekelezeni majukumu yenu ipasavyo, ikiwemo kusimamia mali zote za CCM na jumuiya zake, kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mali za CCM na jumuiya zake, kutoa ushauri juu ya mabadiliko yoyote yanayohitajika katika umiliki wa mali za CCM na jumuiya zake na mutekeleza majukumu mengine ambayo nitakabidhiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Sitarajii kuona dosari za usimamizi wa mali za chama zikiendelea",amesema Magufuli.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza hilo Ndg. Anna Margareth Abdallah amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini na kuwateua kuunda baraza hilo na kumuahidi kuwa watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa umakini na kwa maslahi ya CCM.

"Mambo hayatakuwa kama walivyozoea huko nyuma kwamba kila mtu anamiliki kipande chake cha mali za chama, hapana, mali zote za chama ni mali ya Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi", amesema Anna.

Naye, Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally amesema baraza la hilo ni la kwanza kuundwa baada ya kufanyika marekebisho ya katiba ya CCM, litasimamia mali za CCM pamoja na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya kufuatilia mali za chama ambayo yeye alikuwa mwenyekiti.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad