Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea ameweka wazi kwamba anaamini chama chao kitasimama tena upya licha ya changamoto na migogoro inayoendelea ambayo kwa kiasi kikubwa imeleta mpasuko mkubwa ndani ya chama.
Akizungumza na www.eatv.tv, Mtolea amesema kwamba bado anaamini meza ya mahakama inaweza kuwa suluhisho la migogoro ya Chama chao ambayo imedumu kwa takribani miaka mitatu sasa.
Mtolea ambaye ni Mbunge asiyemuunga mkono Prof. Ibrahim Lipumba amesema kwamba, anaamini vyama vingi vina migogoro, na kwamba hakuna chama kisicho na migogoro kwa kuwa wanasiasa wanakuwa na mitazamo tofauti.
"Sisi tusiomtambua Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF, tunaaamini zaidi kwenye utawala wa sheria tunaamini kwamba mahakama itatusaidia kumaliza mgogoro wetu na tutasimama kuwa wapya na imara zaidi kama awali. Kwa sasa siwezi kutoa maamuzi ya kwamba upande flani utashinda au utashindwa ila kesi zilizopo mahakamani ndizo zitakazoamua hatima ya chama chetu. Matatizo ni sehemu ya changamoto kwenye siasa Chama kisicho na migogoro kinaweza kuwa na watu wa ajabu sana. Tupo kwenye siasa kwa kuwa tunaamini tuna mawazo tofauti na maoni tofauti, hivyo kutofautina kwa mawazo hakujawahi kuwa mgogoro wa kudumu." Mtolea
Akizungumzia kuhusu mtu mmoja (Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya) kuonekana kuwa na mamlaka ndani ya chama chao, Mtolea amesema hayo yote yanasababishwa na udhaifu wa serikali ndiyo maana mwanamama huyo anaonekana na nguvu.
"Siyo kwamba Sakaya ananguvu ya kukiendesha chama lakini serikali kwa kuwa ni dhaifu ndiyo maana inaonekana hivyo, kwa mfanoo kitendo cha Mkurugenzi kukubali kuvuliwa uanachama kwa madiwani wetu Tanga ni udhaifu kwani fika ilikuwa inafahamika kuwa chama kina matatizo na kesi takribani 13 zipo mahakamani" Mtolea
Chama cha CUF kilianza kuwa na mgogoro mwaka 2016 baada ya Mwenyekiti wao Prof. Ibrahim Lipumba kutangaza kurejea kwenye nafasi yake ya uongozi ambayo alijiuzulu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.