Mahakama Yatoa Siku Sita Kesi ya Mpemba wa Meno ya Tembo

Mahakama Yatoa Siku Sita Kesi ya Mpemba wa Meno ya Tembo
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapa siku sita upande wa mashtaka, kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo waliyopewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), katika kesi ya Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli.

Amri hiyo imetolewa  leo  Julai 20 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, muda mfupi  baada ya upande wa mashtaka kuieleza  mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wanalifanyia kazi jalada la kesi hiyo, baada ya kupewa maelekezo na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Yusuph na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh 785.6milioni.

“Nimewapa siku sita kuanzia leo  Julai 20 hadi Jumanne ya wiki ijayo, muwe mmekuja na majibu, mmefikia hatua gani katika kesi hii,  sitawaelewa msipokuja na majibu," amesema Hakimu Simba.

Awali, Wakili wa Serikali Elizabeth Shekunde, alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, Wakili wa Utetezi NehemiaNkoko, alidai kuwa ahadi za upande wa mashtaka katika kesi hiyo ni za kawaida, hivyo wanaomba kujua washtakiwa hao watasomewa lini maelezo ya mashahidi.

“Tunataka kujua wateja wetu watasomewa lini maelezo ya mashahidi na vilelelezo, kwa sababu kila siku, upande wa mashtaka wanakuja na taarifa zile zile," amedai Nkoko.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, mwaka huu itakapotajwa.

Julai 5, Mwaka huu, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa wanalifanyia kazi jalada la kesi hiyo, baada ya kupewa maelekezo na  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Upande huo wa mashtaka alidai kuwa limeshapitiwa na DPP na walipewa maelekezo ambayo wanayafanyia kazi na kwamba wapo katika hatua za kukamilisha maelekezo hayo.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh 785.6milioni na upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad