Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Paul Makonda amempongeza Rais Dkt,John Magufuli kwa kufanikisha zoezi la utiaji saini baina ya serikali ya Tanzania na Korea Kusini.
Mh. Makonda ametoa pongezi hizo kupitia andiko lake alilolitoa saa chache mara baada ya zoezi hilo kukamilika ambalo liko hapo chini.
"Kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam napenda kumpongeza Rais wetu Mpendwa Dkt. John Magufuli kwa kufanikisha utilianaji saini Baina ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini kuashiria kuanza kwa ujenzi wa Daraja la Salender litakaloanzia Coco Beach hadi Agha Khan hospital kupitia bahari ya Hindi ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la msongamano wa magari lililokuwa likipelekea upotevu wa mabilioni ya shilingi.
"Rais Dkt. John Magufuli ameamua kutujengea Daraja hili la kisasa baada ya kujionea adha ya foleni inayowasumbua watumiaji wa Daraja lililopo sasa ambalo kimsingi ni finyu na haliwezi kumudu idadi kubwa ya magari yaliyopo sasa.
Mbali na *kupunguza foleni ujenzi wa daraja hili la kisasa litasaidia kuboresha mandhari ya Jiji letu la Dar es salaam huku wananchi tukiombwa kuendelea kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi na kuendelea kuweka jiji letu safi kwani mji wetu Ndio kitovu cha biashara na uchumi wa taifa letu.
Ujenzi wa *Daraja la Salender utagharimu zaidi ya Shilingi Billion 250 ambapo itachukuwa muda wa miezi 36 hadi kukamilika na litakuwa na urefu wa Km 1.03 kwa upande wa baharini huku likiwa na uwezo wa kuhimili zaidi ya Tani 180 kwa wakati mmoja na magari zaidi ya 55,000 kwa siku.
HAKIKA HUU NDIO UTEKELEZAJI WA YALE ULIYOWAAHIDI WANANCHI KUPITIA ILANI YA CCM."