Makonda Atangaza Nafasi za Kazi Kwa Vijana


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amewataka vijana waliomaliza mafunzo ya JKT na Mgambo na hawana kazi kufika ofisini kwake Ijumaa ya Juli 06, 2018 kwaajili ya kupatiwa ajira ya kusimamia usafi na kuwatoza faini vinara wa uchafuzi wa mazingira.

Makonda ameeleza hayo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaama na kusema katika fedha itakayotozwa kwa wachafuzi wa mazingia asilimia 50 itaenda kwenye halmashauri na asilimia 50 nyingine itaenda kwa vijana wa JKT na Mgambo ambapo kabla vijana hao hawajakabidhiwa jukumu hilo watapewa mafunzo ya sheria ya usafi.

Aidha, Makonda ameagiza makampuni yote yaliyopewa tenda ya usafi Dar es salaam kuanzia ngazi ya mitaa, kata na halmashauri kufika ofisini kwake Jumatano ya Juli 04 wakiwa na mikataba yao kwaajili ya kujiridhisha uwezo wao wa kufanya kazi baada ya uchunguzi aliofanya kubaini uwepo wa kampuni zilizopewa tenda Kubwa wakati hawana vifaa vya kutosha.

Hata hivyo RC Makonda ameziagiza Manispaa zote za jiji hilo kuhakikisha kila mfanyabiashara na vituo vya daladala vinakuwa na sehemu ya kuweka taka 'dustbin'.

Pamoja na hayo, Paul Makonda ametangaza fursa kwa wadau wenye vyoo vya kuhama 'mobile toilet' kufika ofisini kwake ili wakutanishwe na halmashauri wawekeane makubaliano ya ushirikiano ili kuondoa tabia ya watu kujisaidia kwenye kuta na vichochoro.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad