MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ametaja eneo hatari kwa viongozi na sababu za viongozi wa kitaifa akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda kuwekewa mitego ya mawe na misumari inayohatarisha misafara yao wanapotembelea mkoa huo.
Malima aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kuwekewa mtego wa mawe na misumari katika msafara wake ambapo alisema hiyo siyo mara ya kwanza kwa viongozi kufanyiwa mambo hayo kwani hata Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda aliwahi kufanyiwa hivyo.
Alisema Pinda aliwekewa mawe wakati akiwa na tume iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuatilia mgogoro wa ardhi katika eneo hilo. Malima alisema wanaoweka mitego hiyo ya mawe na misumari barabarani ni wanavijiji waliowahi kuripotiwa mara nyingi na uongozi wa hifadhi hiyo kuwa ni wa vijiji jirani ambao hujaza mawe barabarani akitaja sababu kuwa ni kuzuia magari ya doria ili waweze kulisha mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo.
Akiwa njiani majira ya saa tatu za usiku kwenye gari la wazi baada ya kukagua eneo hilo la mpaka kwa zaidi ya saa sita, Waziri Kigwangalla na msafara wake walikuta lundo la mawe yakiwa barabarani ndani ya eneo la hifadhi hiyo, hali iliyosababisha taharuki kubwa na waliokuwa katika msafara wake ilibidi kushuka na kuanza kuondoa mawe hayo ili kupata njia ya kupita.
Awali, kabla ya tukio hilo la mawe barabarani, moja ya gari lililokuwa likiongoza msafara huo lilipata pancha baada ya kukanyaga misumari iliyokuwa imetegwa kwenye ubao katika moja ya barabara zinazoingia na kutoka ndani ya hifadhi hiyo ya Serengeti. Waziri Kigwangalla alisikitishwa na kitendo hicho ambacho alikielezea kuwa sio cha kiuungwana kwa kuwa kinalenga kudhoofisha juhudi za Serikali kumaliza mgogoro huo kwa faida ya pande zote.
“Mimi ni Muislam, nimesikia kwa masikio yangu na wala sijaambiwa na mtu yeyote na siwezi kumsingizia mtu, nimeshangazwa sana kusikia kuna kiongozi tena mtendaji wa chama tawala anahamasisha uvunjifu wa amani, anawezaje kuitukana Serikali? Hapa sisi tumekuja kuwahudumia wananchi” alisema Dk. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.
Waziri Kigwangalla aliliagiza Jeshi la Polisi Wilaya ya Tarime mkoani Mara kumkamata na kumfungulia mashtaka Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Newton Mongi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Richard Tiboche kwa tuhuma za kuikashifu Serikali na kuchochea mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi ya Serengeti na vijiji jirani kikiwemo Kijiji cha Kegonga.