Malkia wa urembo katika gereza kuu la wanawake la Lang'ata jijini Nairobi amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na kosa la kumuua mpenzi wake.
Ruth Wanjiku Kamande alipatikana na kosa la kumuua mpenzi wake Farid Mohammed katika mtaa wa Buruburu, Nairobi mnamo tarehe 20 Septemba, 2015.
Jaji huyo amesema hukumu hiyo inafaa kuwa funzo kwa vijana ambao wanafaa wafahamu kwamba "si vyema kumuua mpenzi wako, ni vyema kujiondokea ukaenda zako."
Wakati wa kukamatwa kwake, mwanamke huyo mwenye miaka 25 sasa alikuwa ndio tu amejiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea Uanabiashara, kwa mujibu wa wakili wake.
"Mwanamume huyo aliyeuawa aliyekuwa na miaka 24 wakati huo alikuwa mjane na alikuwa anategemewa na jamaa wengine, haki inafaa kutekelezwa," wakili wa mashtaka alisema.
Mwanamke huyo alikuwa amejitetea kortini na kusema mzozo kati yake na marehemu ulizidi baada yake kugundua kadi ya hospitali iliyoashiria kwamba Mohammed alikuwa anapokea matibabu ya Ukimwi.
Alisema alimkaripi kumwuliza ukweli kuhusu hilo na kwa mujibu wake, marehemu alimwambia wakati huo kwamba heri wafe wote kuliko hali yake ya Ukimwi itambulike hadharani.
Bi Kamande anasema mzozo wao ulizidi hata zaidi baada yake kugundua barua za mapenzi kutoka kwa wanawake wengine.
Alisema alimdunga kisu mpenzi wake baada ya kisu cha kutumiwa jikoni kumwangukia wakipigana na hapo akamdunga kisu mara kadha. Anadaiwa kumdunga kisu mpenzi huyo wake mara 22.
Bi Kamande alikuwa ameambia mahakama kwamba marehemu alijaribu pia kumbaka lakini mahakama ilisema uchunguzi wa madaktari ulionyesha hakukuwa na ukweli kuhusu madai hayo.