Mambo Mazuri kwa Ufaransa Yatinga Fainali Kombe la Dunia

Mambo Mazuri kwa Ufaransa Yatinga Fainali Kombe la Dunia
Baada ya usiku huu kushinda mechi yao ya nusu fainali dhidi ya Ubelgiji kwa bao 1-0, Ufaransa sasa imetinga fainali ya kombe la dunia kwa mara ya tatu ndani ya miaka 20 na kuwa taifa lililofika fainali mara nyingi zaidi katika miaka hiyo.


Ufaransa imefanikiwa kutinga hatua ya fainali katika miaka ya 1998 ambapo walitwaa kombe wakiwafunga Brazil kwenye mechi ya fainali, 2006 ambapo walifungwa na Italia na 2018 baada ya leo kushinda bao 1-0 dhidi ya Ubelgiji kwenye nusu fainali.

Kwa upande wake kocha wa kikosi hicho Mfaransa, Didier Deschamps, ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa Ufaransa kufika katika fainali mbili tofauti za mashindano makubwa. Alifika fainali ya EURO 2016 na kupoteza dhidi ya Ureno na amefika fainali ya kombe la dunia 2018.

Kwa upande mwingine walinzi wa kikosi cha Ufaransa mwaka huu Pavard, Varane na Umtiti wote wamefunga katika fainali hizi na kuirudia rekodi ya walinzi Lizarazu, Blanc na Thuram ambao walifunga mabao katika fainali za mwaka 1998.

Naye Antoine Griezmann sasa amehusika kwenye mabao 5 akifunga 3 na kusaidia 2 hivyo kuwa nyuma ya Harry Kane pekee kama mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi katika fainali hizi. Kane amehusika kwenye mabao 6 yote akifunga.

Ufaransa sasa itasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili itakayopigwa kesho kati ya Croatia dhidi ya England, ambapo mshindi ataungana na Ufaransa katika mchezo wa fainali utakaofanyika Julai 15.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad