Mambo ya kujua kuelekea fainali ya kombe la dunia
0
July 15, 2018
Fainali za kombe la dunia mwaka 2018, leo zinafikia tamati kwa mchezo wa fainali kati ya Ufaransa na Croatia utakaopigwa kuanzia saa 12:00 Jioni kwa saa za Moscow na Afrika Mashariki. Uwanja ni Luzhniki jijini Moscow unaoingiza mashabiki 81,000.
Wachezaji wa Croatia (nyekundu na nyeupe) na Ufaransa (blue).
Fainali ya leo ni kumbukumbu ya nusu fainali ya miaka 20 iliyopita, ambayo iliyakutanisha mataifa haya mawili huku Ufaransa ikishinda na kuingia fainali ambako ilicheza na Brazil na kutwaa ubingwa. Ikumbukwe Ufaransa ndio walikuwa wenyeji wa fainali hizo.
Croatia leo wanasaka taji lao la kwanza wakiwa ndio wamefanikiwa kufika fainali kwa mara ya kwanza huku Ufaransa ambao waliwakwamisha katika nusu fainali za mwaka 1998 kwa bao la mlinzi Lilian Thuram wao wanasaka taji la pili wakiwa pia wanacheza fainali yao ya tatu ndani ya miaka 20.
Kocha wa sasa wa Ufaransa Didier Deschamps mwaka 1998, alikuwa ndio nahodha wa Ufaransa na baada ya kutwaa ubingwa kwa mwaka huo leo atakuwa anawania kuifikia rekodi ya makocha Mario Zagallo wa Brazil Franz Beckenbauer na Ujerumani ambao walitwaa kombe wakiwa wachezaji na baadae kama makocha.
Vikosi vinavyotarajiwa kuanza leo.
Ufaransa: Hugo Lloris, Benjamin Pavard, Raphael Varane, Samuel Umtiti, Lucas Hernandez, Paul Pogba, Ngolo Kante, Kylian Mbappe, Antoine Griezmann, Blaise Matuidi na Olivier Giroud.
Croatia: Danijel Subasic, Sime Vrsaljko, Dejan Lovren, Domagoj Vida, Ivan Strinicm, Ivan Rakitic, Marcelo Brozovic, Ante Rebic, Luka Modric, Ivan Perisic, Mario Mandzukic.
EATV
Tags