Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa amewataka watumiaji wa vyombo vya moto kutompigia simu pindi wakamatwapo na askari wa barabarani kwa kuwa yeye ndio amewaagiza kufanya kazi hiyo.
Kamanda Mambosasa ametoa kauli hiyo jana Julai 24, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutaka kila mmoja ambaye anatumia chombo cha moto kufuata sheria zilizowekwa ili kusudi kuepukana na ajali zisizokuwa na ulazima ambazo zinapelekea vifo, ulemavu na utegemezi kwenye familia.
"Ninaomba nisipigiwe simu juu ya kwamba umekamatwa kwa kosa la usalama barabarani bali unipigie tu pale unahisi umeonewa. Kwa kuwa wengi wao wanaopigia simu wametenda makosa ninaomba nisipigiwe kwasababu mimi ndio nawatuma wawakamate", alisema Kamanda Mambosasa.
Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa amliendelea kwa kusema; "Jeshi la Polisi tunaendelea kuhimiza watu kufuata sheria za usalama barabarani, makosa haya yanafanya watu walalamike kwamba wanakamatwa sana lakini cha ajabu watu wanaendelea kutenda makosa sana. Bodaboda bado ni tatizo tunawashuhudia kwenye vivuko 'zebra cross' lakini hata matumizi ya barabara ya mwendokasi wanavamia na kufanya wanavyotaka".
Kauli hiyo ya Mambosasa imekuja baada ya kuwepo kwa madereva wa vyombo hivyo kufanya makosa ya barabarani kwa makusudi kwa kujua yupo mtetezi wao ambaye ataweza kuwasaidia mara wanapokuwa wamesimamishwa na kukamatwa barabarani.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam kupitia Kikosi chake cha Usalama barabarani kuanzia Juni 01 hadi Juni 3 mwaka huu wamefanikiwa kukamata jumla ya magari 42,488 na pikipiki 1,941 kutokana na makosa 73 ya usalama barabarani na kuingizia mapato Jeshi la Polisi takribani shilingi Bilioni 2.15 kama tozo zitokanazo na madereva kukiuka sheria za usalama barabarani.