Masheikh Waonywa Kuozesha Wabakwaji

Masheikh waonywa kuozesha wabakwaji
Masheikh kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kuwaozesha wanaume watoto waliobakwa na kupata ujauzito, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchochea vitendo hivyo.

Akizungumza katika mafunzo ya udhalilishaji wa kijinsia na njia mbadala ya kupambana nazo juzi, mwezeshaji Shukri Gesod alisema tabia ya kuwaozesha watoto wenye ujauzito, haikubaliki katika sheria ya dini, hivyo ni vyema masheikh wakaepuka jambo hilo.

Gesod alieleza kuwa iwapo masheikh, wataendelea kuwaoza watoto hao, vitendo vya ubakaji vitaongezeka kwa kuwa hiyo ni njia mojawapo inayosababisha vikithiri.

“Kwa kweli haikubaliki kwa mtoto aliyebakwa na kusababishiwa ujauzito kuozwa mume, itakuwa hamtendei haki kutokana na alichofanyiwa, masheikh ndiyo mnaoozesha tuache kabisa tabia hiyo,” alisema.

Imamu kutoka Chakechake, Machano Ame Faki alisema wazazi wamekuwa na tabia ya kusuluhisha mtoto wao anapobakwa kisha kumuoza, jambo ambalo linasababisha kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Naye Amira wa Jimbo la Gando, Salma Khamis Juma alisema wamefarijika kupata mafunzo hayo na kwamba, yatawasaidia kujua mbinu mbalimbali za kuweza kuwafikishia elimu wanajamii ili kuhakikisha tatizo hilo linaondoka kabisa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad