DAR: Hatma ya staa wa filamu Bongo, Wema Isac Sepetu katika midani za siasa nchini, imeingia dosari kutokana na hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Shilingi milioni 2 iliyotolewa juzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi yake.
Wema ana ndoto ya kuwa mwanasiasa, hususan katika nafasi ya ubunge. Mwaka 2015 msanii huyo alienda mkoani Singida kugombea ubunge kupitia viti maalumu vijana, lakini alikosa.Pamoja na matokeo hayo, watu walio karibu na mrembo huyo, wamekuwa wakieleza kuwa bado ana ndoto ya kurudi kwenye kinyang’anyiro cha siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hata hivyo, hukumu iliyotolewa juzi dhidi yake baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kutumia madawa ya kulevya aina ya bangi, imemwondolea sifa ya kugombea ubunge na kuwa kiongozi wa umma. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kifungu 67 (2)c na d, inasema kuwa, ikiwa mtu amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na kupewa adhabu ya kifo au kufungwa gerezani kwa muda usiopungua miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote linaloambatana na utovu wa uaminifu, hataruhusiwa kugombea uongozi wa umma.
Katiba hiyo imebainisha pia kuwa ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya uchaguzi mkuu kama mtu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungu kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma hataruhusiwa kuwania uongozi.Mwanasheria maarufu nchini Emmanuel Elias alithibitisha kuwa kwa kosa na adhabu aliyopata Wema, anaweza asiruhusiwe kugombea uongozi wa umma kama atawekewa kipingamizi.
“Ninachojua kuna sheria inayozungumzia suala hilo, kwamba kama mtu amethibitika kufanya kosa na Mahakama ikamwadhibu kwa kifungo kinachozidi miezi sita atazuiwa kugombea uongozi, na hili ni suala la kikatiba,” alisema Elias.Ijumaa Wikienda lililokuwepo mahakamani siku ya hukumu ya kesi ya Wema, lilibahatika kunasa sauti ya jaji mmoja ambaye pia alieleza jinsi ambavyo kuna ugumu Wema kuwania nafasi za kisiasa.
“Yaani Wema ni kipenzi sana cha watu lakini kutokana na kuhukumiwa zaidi ya miezi sita basi amepoteza nafasi yake hiyo ambayo naamini kabisa mwaka 2020 angeweza kupata ubunge bila kipingamizi kikubwa,” alisikika jaji huyo akizungumza nje ya mahakama siku ambayo Wema alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, lakini akalipa faini ya Shilingi milioni 2.
Hata hivyo, baadhi ya wanasheria wameleeza kuwa uzuri wa sheria ni kung’ata pande zote. Wakasema Wema anaweza akagombea tena kama atakata rufaa kupinga hukumu hiyo na kufanikiwa kushinda tena kesi hiyo.
Katika hatua nyingine, staa wa filamu Bongo, Kajala Masanja ametoa sababu za kutokuwa mstari wa mbele kumlipia faini staa mwenzake Wema Sepetu, kama Wema alivyomlipia yeye faini ya Shilingi milioni 13 ili asiende jela miaka saba miaka ya nyuma.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Kajala ambaye kwa sasa yupo nchini Dubai, alisema kuwa kama angetakiwa kusaidia kumlipia Wema faini hiyo asingekuwa na tatizo, angemlipia.
“Ningejua na kuwa na hakika Wema hawezi kulipa hiyo faini, ningemlipia hata kama ni kwa kukopa hizo pesa, lakini mimi sikuwepo nchini wakati Wema anahukumiwa,” alisema.
Hata hivyo Kajala ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa zinazosambaa kuwa amemtelekeza rafiki yake Wema akisema; “Jamani mimi naona watu wanasema sikuonekana mahakamani, lakini hawajui kama nipo au sipo, hata hivyo kama ingehitaji faini ambayo kubwa kwa kweli mimi nisingeshindwa hata ya kukopa ningemlipia.”
Kajala alisisitiza; “Sio kwamba sikuwa napenda kwenda mahakamani kuungana naye, kulikuwa na vitu vinaendelea kwa upande wangu hivyo ikaniwia vigumu.”
STORI: Imelda Mtema, DAR
Maskini...Ndoto ya Wema Sepetu ya Kupata Ubunge Basi Tena
0
July 24, 2018
Tags