MASTAA wa dunia, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wametupwa nje ya Fainali za Kombe la Dunia baada ya timu zao za Ureno na Argentina kufungwa jana Jumamosi kwenye mechi za mtoano.
Vipigo hivyo vimepoteza ndoto za wakali hao wawili kutwaa Kombe la Dunia kwani umri unazidi kuwatupa mkono huku Ronaldo akiwa na umri wa miaka 33 wakati mwenzake Messi ana 31.
Watu wengi wanaamini kuwa fainali huenda zikawa za mwisho kwa mastaa hao, ambao wametwaa mataji mengi na klabu zao za Real Madrid na Barcelona za Hispania lakini hawajaweza kutwaa Kombe la Dunia.
Ufaransa na Uruguay sasa zitakabiliana kwenye robo fainali Ijumaa ijayo baada ya kuibuka kidedea kwenye mechi zao za mtoano jana. Straika wa Uruguay, Edinson Cavani ndio alizima ndoto za Ronaldo za kusonga mbele kwenye Kombe la Dunia baada ya kuifungia timu yake mabao mawili ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ureno kwenye Uwanja wa Fisht mjini Sochi.
Cavani alipachika bao la kwanza katika dakika ya saba baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Luis Suarez lakini Ureno ilisawazisha katika dakika ya 55 kwa bao lililofungwa na beki Pepe kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Guerreiro.
Cavani, ambaye aliumia na kutoka nje, aliongeza bao la pili baada ya kupokea pasi akiwa mwenyewe pembeni ya goli akapiga shuti kali lililotinga wavuni mnamo dakika ya 62.
Nayo Ufaransa ilikata tiketi ya robo fainali baada ya kuinyuka Argentina mabao 4-3 kwenye mechi ya mtoano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kazan Arena. Straika yosso wa Ufaransa, Kylian Mbappe ndio alikuwa nyota wa mchezo huo kutokana na kufunga mabao mawili. Pamoja na kufunga mabao mawili lakini Mbappe alisababisha penalti iliyozaa bao