Maswali mengi yameachwa bila majibu baada ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, kutoa taarifa kuwa maafisa wa polisi ambao walikuwa wakishikiliwa kwa shutuma za mauaji ya mwanafunzi Akwilina Akwiline, wameachiwa huru.
Sababu za kuachiwa kwao imeelezwa kuwa ni ushahidi hafifu dhidi yao kuweza kutiwa hatiani.
''Hivyo ndivyo ilivyo Baada ya upelelezi, jalada lilikwenda kwa mwanasheria naye amerudisha na maelekezo hayo kuwa ushahidi ni hafifu, hizi ni taratibu za kawaida nchini kwetu wanaoshangaa labda ni hao walio nje ya nchi yetu'' Alieleza kamanda Mambosasa alipozungumza na BBC.
Akwilina, mwanafunzi wa chuo kikuu alipigwa risasi wakati Polisi walipokuwa wakidhibiti maandamano ya upinzani jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu.
Makundi ya kiraia Tanzania yaomba kuundwe tume ya kuchunguza mauaji
Kifo chake kilikuwa gumzo baadhi ya watu wakighadhabishwa na jinsi jeshi la polisi lilivyotumia nguvu kukabiliana na maandamano nchini.
'Ni nani aliyemuua Akwilina?'
Kumekuwa na maoni kadha wa kadha kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuachiwa kwa askari waliokuwa wakishikiliwa
Wengine wakiuliza ni nani sasa alimuua Akwilina?
Wakati wa tukio hilo walioshuhudia walisema kuwa maafisa wa polisi walitumia vitoa machozi na risasi katika harakati za kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha Chadema waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya tume ya uchaguzi.
Mwanafunzi huyo ambaye jina lake na picha vilisambazwa katika mitando ya kijamii alipigwa risasi akiwa ndani ya basi dogo maarufu kama daladala jijini Dar es salaam, ikiwa siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la kinondoni kufanyika.
Rais wa Tanzania John Magufuli aliviagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuwachukulia hatua waliosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji Tanzania, NIT, Akwilina Akwiline.
"Nimesikitishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilini wa Chuo cha Usafirishaji (NIT). Natoa pole kwa familia,ndugu,wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huu. Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili," Rais Magufuli aliandika kwenye mtandao wa Twitter.
BBC