Mbunge Afikishwa Mahakamani Kwa Utapeli


Mbunge wa zamani wa Dimani – Zanzibar (CCM), Abdallah Sharia Ameir (54) na mwenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kujipatia Sh55 milioni kwa njia ya udangan yifu.


Mbali na Ameir ambaye ni mkazi wa Mnazi mmoja, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ya jinai namba 229 ya mwaka 2018 ni Dk Athuman Rajabu (32).


Wakili wa Serikali, Janeth Magohe leo Alhamisi Julai 12, 2018 amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Hamisi Ally kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kati ya Julai 17 na Septemba 26, 2017 jijini Dar es Salaam.


Wakili Magohe amedai washtakiwa walijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Abdi Hirsi Warsame wakiahidi kuwa wangemsambazia vifaa tiba katika hospitali, wakati wakijua kuwa ni uongo.


Washtakiwa wamekana shtaka na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.


"Upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha upelelezi,” amesema wakili huyo.


Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo wakili wa utetezi, Thimotheo Wandiba ameiomba mahakama kuwapatia dhamana wateja wake kwa sababu shtaka lao linadhaminika.


"Naomba mahakama yako iwapatie dhamana wateja wangu kwani shtaka lao linadhaminika,” amedai wakili Wandiba.


Hakimu Ally ametaja masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh27.5 milioni kila mmoja.


Pia, wadhamini wao wanatakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh27.5 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.


Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande. Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho, Julai 13 itakapotajwa kwa ajili ya dhamana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad