Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara 'Bwege' (CUF), ameweka wazi kuwa endapo angekuwa Rais wa nchi basi asingeweza kumuacha Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, katika baraza lake la mawaziri.
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu
Akizungumza katika kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka kila Jumatano kupitia ukurasa wa Facebook EATV, Mh. Bungara amesema kwamba anaamini Tundu Lissu anafaa sana kuwa kwenye Wizara ya Katiba na Sheria, hivyo lazima angempa nafasi hiyo kwa kuwa angeitendea haki.
Aidha Mbunge huyo aliongeza kwamba, ingawa wabunge wengi kutoka UKAWA wana uwezo lakini kama pia asingemuacha Mbunge wa Tandahimba, Katani Hamad Katani, katika wiazara ya Kilimo kwa kuwa naye ana uwezo wa kuongoza wizara hiyo, hivyo angeweza kutatua changamoto za wakulima.
Akifafanua kuhusu Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Musukuma, kama endapo angehamia katika chama chake wizara ambayo ingemfaa amesema "wizara ambayo ningempa Musukuma na ingemfaa ingekuwa ni ya Utamaduni".
Akizungumzia kuhusu mawaziri anaowakubali katika serikali iliyopo madarakani, Mbunge Bungara amesema kwamba "Lukuvi namkubali sana. Alitatua mgogoro jimboni kwangu uliodumu kwa miaka 40, mawaziri wote waliopita walishindwa. Lukuvi mkweli, hana hofu akitekeleza majukumu yake viongozi waliopita walikuwa wakifika wanapewa mchele kuku wanaondoka. Sifa za kiongozi ni ukweli na uaminifu, nyeusi anasema nyeusi na nyeupe ni nyeupe".
Aidha, Mh. Bungara amesema anamkubali Waziri Suleiman Jafo na ubora wake ni kwamba hababaishi majibu pale anapoulizwa swali tofauti na mawaziri wengine.