Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka amekamatwa na Polisi akiwa kwenye kituo kikuu cha polisi Tunduma alikokwenda kuomba ulinzi.
Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga amesema mbali na Mwakajoka, pia Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Songwe, Ayub Sikagonamo naye amekamatwa.
“Pia wapo baadhi ya madiwani, wanachama wa Chadema na walinzi wa chama nao wamekamatwa,” amesema.
Amesema Mwakajoka na Sikagonamo leo asubuhi walipanga kwenda ofisi za Halmashauri ya Tunduma kwa ajili ya kuchukua fomu za wagombea wa udiwani katika kata tano, lakini ofisi hizo zilikuwa zimezingirwa na polisi.
“Kutokana na hali hiyo Mwakajoka akiwa na Sikagonamo waliona kuliko kwenda eneo hilo na kuonekana wanakwenda kufanya vurugu, waliamua kwenda kuonana na mkuu wa kituo ili awape ulinzi wa askari,” amesema Hainga.
“Ila walipofika (Mwakojoka) alielezwa kuwa jana usiku alifanya kikao na wenzake kwa lengo la kufanya maandamano hivyo anawekwa chini ya ulinzi, basi wakawekwa ndani hadi muda huu.”
Amesema hatua waliyoichukua ni kuwasiliana na uongozi wa juu wa chama hicho sambamba na kufanya taratibu za dhamana.
Haonga amesema hadi leo saa 7 mchana hakukuwa na mgombea udiwani wa Chadema aliyechukua fomu ya kugombea kwa kile alichokiita mizengwe inayofanyika, ikiwa ni pamoja na kukamatwa lwa wagombea walioteuliwa na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.