Wakala wa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umesema watumiaji wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya ya kuweka bangi kwenye keki kutokana na kudhibitiwa kutumia katika maeneo mengine.
Mbali na kutumia keki kuweka dawa hizo, pia wanatumia dawa tiba za binadamu kuondoa uraibu wa dawa.
Kauli hiyo imetolewa na kaimu mkurugenzi idara ya sayansi jinai na huduma za vinasaba, David Elias kwenye banda la wakala huo lililopo kwenye maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini hapa.
Huku akiionyesha, “hii ni keki Polisi waliikamata na kutilia shaka hivyo ikaletwa kwetu kwa ajili ya vipimo, tulichobaini ndani mlikuwa na kiasi kikubwa cha bangi.”
Amewataka wazazi kuwa makini na hafla mbalimbali za vijana kwa maelezo kuwa maeneo hayo ndio kimbilio la watumiaji hao, baada ya kudhibitiwa katika maeneo mengine.