Merkel Abadilisha Msimamo Kuhusu Uhamiaji

Baada ya vuta nikuvute ya kuda mrefu, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na waziri wake wa mambo ya ndani, Horst Zeehofer, wamekubaliana kuondosha tofauti zao kuhusiana na sera ya uhamiaji.

Merkel amesema Ujerumani itawazuia wahamiaji waliosajiliwa katika nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya kwenye vituo maalumu, huku mchakato wa kutafuta njia za kuwarejesha makwao ukiendelea.

Wachambuzi wanasema Merkel amechukua hatua hiyo ili kuunusuru utawala wake.

Baadhi walikuwa wamesema kuwa iwapo Merkel hangechukua uamuzi huo, serikali ya muungano anayoiongoza sasa ingekuwa katika hatari ya kusambaratika na uongozi wake kufika kikomo.

Kiongozi huyo aidha amesifu makubaliano yaliyoafikiwa na washirika wake wa jimbo la Bavaria ambao walikuwa wametishia kujiondoa kutoka serikali yake ya mseto.

Kwendelea kushirikiana kwa vyama vya Christian Social Union, CSU, na Christian Democratic Union, CDU, kumetajwa na wachambuzi kama ambako kutasaidia kulinda kanuni ya uhuru wa watu kutembea katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kuiruhusu Ujerumani kuchukua hatua katika ngazi ya kitaifa kupunguza na kudhibiti idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaowasili kwenye nchi hizo.

Katika kauli ambayo iliwashangaza wengi siku ya Jumatatu, Merkel aliwaambia waandishi wa habari kwamba pamoja na kujenga vituo vya muda vya wahamiaji, Ujerumani pia itatafuta njia za kuwarejesha makwao chini ya makubaliano na nchi wanakotokea waomba hifadhi na ambako tayari wamesajiliwa.

Kwa muda mrefu, Merkel, ambaye, kwa mara ya kwanza aliingiaa mamlakani mwaka wa 2005, amekuwa katika mstari wa mbele kuunga mkono sera ya uhamiaji inayoruhusu wakimbizi na wahamiaji kupata hifadhi katika nchi za bara ulaya, ikiwemo Ujerumani.

Manamo mwaka wa 2015, Merkel alichukua hatua iliyoibua utata, ya kuwaruhusu wahamiaji Zaidi ya milioni moja, kuingia nchini kwake, wengi wao wakitokea nchi kama vile Syria, Iraq na Afghanistan.

VOA imezungumza na mchambuzi wa masuala ya siasa na mwandishi wa habari mstaafu, Ramadhan Ali, akiwa mjini Berlin, Ujerumani, na kwanza ikamuuliza kueleza ni nini ambacho huenda kimepelekea Kansela Merkel kuchukua hatua hiyo ambayo ni tofauti kabisa na sera zake kuhusu uhamiaji, pamoja na masimamo ambao amaekuwa akishikilia kwa muda mrefu.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad