Mfahamu Samuel Umtiti aliyewafikisha Ufaransa fainali Kombe la Dunia

Ufaransa watakutana na mshindi kati ya England na Croatia kwenye fainali ya Kombe la Dunia nchini Urusi baada ya kuwashinda majirani wao Ubelgiji kwenye nusufainali mjini St Petersburg.

Mechi ya fainali itachezwa Jumapili uwanjani Lzhiniki mjini Moscow saa tatu usiku saa za Afrika Mashariki.

Ubelgiji wamesalia na mechi moja ya kuamua atakayemaliza wa tatu, mechi ambayo itachezwa Jumamosi.

Bao pekee la mechi ya nusu fainali lilifungwa na beki Samuel Umtiti baada ya kona iliyopigwa na Antoine Griezmann.

Mchezaji huyu aliyewavusha Ufaransa hadi fainali ni nani?
Samuel Yves Umtiti huchezea klabu ya Barcelona ya Uhispania.

Ni mchezaji wa miaka 24 ambaye alizaliwa mnamo 14 Novemba mwaka 1993 mjini Yaounde, Cameroon. Mamake ni Annie Ngo Um lakini babake hajulikani ni nani. Ana ndugu kwa jina Yannick Umtiti.

Yeye kwa kawaida huwa ni beki wa kati.

Ni mchezaji mrefu kwa kimo, kimo chake ni futi sita (1.83m) jambo ambalo huenda lilimsaidia katika kufunga bao la kichwa dhidi ya Ubelgiji ambapo alikuwa anakamiliana na mchezaji mwingine mrefu wa kimo anayefahamika sana kwa mipira ya kichwa, Marouane Fellaini.

Kutokana na kwamba alizaliwa Cameroon, ni mchezaji ambaye alikuwa na fursa ya kuichezea timu ya taifa ya Cameroon. Ana uraia wa Cameroon na Ufaransa.


Juhudi za Shirikisho la Soka la Cameroon na nyota wao wa zamani wa kimataifa Roger Milla za kumshawishi aiwakilishe Cameroon hazikufua dafu.

Alizaliwa katika maisha ya umaskini na alikuwa tu ndio ameanza kuzoea maisha ya Yaounde pale familia aliyokuwa anaishi nayo ilipofunganya virago na kuhamia Ufaransa katika viunga vya mji wa Lyon. Kutokana na ufukara mamake alikuwa amemkabidhi kwa jamaa aishi naye akiwa bado mdogo. Kuna utata hata hivyo kuhusu iwapo alisafiri na jamaa waliokuwa wanamlea au na mamake mara ya kwanza kwenda Ufaransa.

Baada ya kukaa miezi kadha Villeurbanne ambapo alilelewa katika jamii ya wahamiaji kutoka Cameroon, hatimaye walihamia Menival.


 Mwaka aliohamia Ufaransa, 1995, ilikuwa si muda mrefu sana baada ya Roger Milla kuvuma sana akichezea Cameroon jambo ambalo lilichochea wahamiaji wengi wa Afrika waliokuwa nchini Ufaransa kukumbatia kandanda. Ni kipindi hicho ambapo wachezaji nyota kama vile Paul Pogba, Raphael Varane na Romelu Lukaku walikuwa watoto.

Umtiti alianza kuonyesha ustadi wa kusakata gozi akiwa na miaka mitano hivi ambapo kwa makubaliano kati ya shule yake na mamake aliruhusiwa kuifuata ndoto yake.

Njiani kati ya nyumbani kwao na shuleni kulikuwa na uwanja wa klabu ya soka ya Menival FC na huko ndiko alipoanza kuchezea soka.

Jinsi Kylian Mbappe alivyofikia umaarufu wake
Rais wa zamani wa klabu hiyo Said Intidam anamkumbuka: "Alikuwa na miaka mitano tu lakini angeweza kucheza katika mchezo wa wachezaji 11 kila upande bila matatizo."

Rais wa sasa wa klabu hiyo Judi Bouzama anasema tofauti kati yake na wachezaji wengine ilionekana wazi.

Haki miliki ya pichaAFP
"Hakuwa mchezaji wa kiwango cha Menival, alikuwa i mchezaji wa klabu kubwa kama vile Olympique Lyonnais au Saint-Etienne," amenukuliwa na mtandao wa SportEnglish.

Alianza kwenda Lyon kujifunza soka akiwa na miaka tisa mwaka 2001 na kuibuka kuwa miongoni mwa wachezaji nyota katika kikisi cha wachezaji chipukizi.

Alianza kama mshambuliaji, baadaye akawa anacheza safu ya kati kabla ya mwishowe kuanza kucheza kama beki.

Baada ya kukaa miaka 11 akijifunza soka akademi ya Lyon, aliichezea timu kubwa ya klabu hiyo mara ya kwanza Januari 2012 na kufikia msimu wa 2015/16 alitawazwa mchezaji bora wa msimu na mashabiki wa klabu hiyo ambapo alimshinda Alexandre Lacazette ambaye kwa sasa huichezea Arsenal.

Alikuwa amewachezea mechi 170 za ushindani na kufunga mabao matano, na kusaidia ufungaji wa mabao mengine mawili.

Ni beki stadi ambaye kipaji chake kilitambuliwa na Barcelona na akanunuliwa €25 milioni (£21.2 milioni) Julai mwaka 2016 kutoka Olympique Lyonnais (Lyon) ya Ufaransa ambapo alikuwa mchezaji wa kutegemewa sana.

Umtiti alitafutwa na Barcelona kuimarisha safu yao ya ulinzi na zaidi kujaza pengo lililoachwa na nyota Carles Puyol baada ya Jeremy Mathieu na Thomas Vermaelen kuonekana kutoimudu vyema kazi hiyo.

Mashabiki wa Ufaransa wakisherehekea kufika fainali Kombe la Dunia katika barabara za Paris
Alichezea Barcelona mara ya kwanza 17 Agosti 2016 katika mechi ya Super Cup ya Uhispania ambapo walishinda 3-0 dhidi ya Sevilla. Aliwafungia bao la kwanza 4 Machi 2017 dhidi ya Celta de Vigo. Siku zilivyosonga, aliunda ushirikiano wa karibu sana na Gerard Pique na Jordi Alba katika safu ya ulinzi na alikuwa katika timu iliyofanikiwa kuandikisha historia kwa kujikwamua dhidi ya Paris Saint Germain Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2017 baada ya kushindwa 4-0 mechi ya kwanza lakini wakashinda 6-1 mechi ya marudiano.

Alishinda Copa Del Rey 2016-17 akiwa na wachezaji wengine kama vile Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez Barcelona.

Kuichezea timu ya taifa
Umtiti aliitwa kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa katika Euro 2016 ambapo Ufaransa walikuwa wenyeji ambapo aliwekwa kikosi na Didier Deschamps baada ya kuumia kwa Jeremy Mathieu.

Aliwachezea mara ya kwanza michuano hiyo hatua ya robofainali dhidi ya Iceland baada ya beki wao mwingine Adil Rami kupigwa marufuku kucheza mechi moja.


Uchezaji wake mzuri ulimfanya kuchezeshwa kikosi cha kuanza mechi na kwa kipindi kilichosalia michuano hiyo. Alicheza nusufainali dhidi ya Ujerumani na kwenye fainali waliposhindwa na Ureno.

Alikuwa ndiye mchezaji wa kwanza wa ndani uwanjani tangu Gabriel De Michele katika Kombe la Dunia 1966 kuchezeshwa mara ya kwanza katika timu ya taifa wakati wa michuano mikubwa.

Umtiti alijiunga na Barcelona mwaka 2016
Aliwafungia Ufaransa bao lake la kwanza 13 Juni 2017 kwa kuwasawazishia dhidi ya England mjini Paris katika mechi ambayo walishinda 3-2.

Kabla ya kujiunga na timu kuu ya taifa, alikuwa amecheza katika timu za taifa za wachezaji chipukizi mara 47 na kufunga mabao matatu.

Anasemaje kuhusu Cameroon?
Bado hajakata uhusiano wake na taifa hilo la Afrika.

Kwenye mahojiano na FranceFootball, alisema: "Bado nina jamaa Yaounde na bado huwa twawasiliana kwa simu, lakini sina kumbukumbu nyingi kuhusu maisha yangu ya miaka miwili huko Cameroon," alisema.

"Nimezuru huko mara mbili, ni sehemu ya miziz yangu. Shirikisho lao la soka liliniomba niichezee Cameroon mara kadha, washauri wangu walikutana na Roger Milla kutokana na ombi lake, kwa heshima. Walisikiliza maoni yangu, lakini hakukuwa na mabadiliko yooyte. Nilikuwa tayari nimefanya uamuzi wangu, nilikuwa nimeufikiria vyema.

"Tangu mwanzoni, nilitaka kuichezea Ufaransa. Sijui kama Cameroon walikerwa na uamuzi wangu, lakini niliufanya uamuzi wangu na lazima uheshimiwe, watu wapende wasipende."

Uhusiano na Mitandao ya kijamii
Mchezaji huyu bado hajafunga ndoa rasmi lakini anadaiwa kuwa na uhusiano na Alexandra Dualauroy mwenye asili ya Colombia.

Ruka ujumbe wa Instagram wa samumtitiMwisho wa ujumbe wa Instagram wa samumtiti
Umtiti ana wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii na hasa Instagram ambapo kufikia sasa ana wafuasi 4.1 milioni.

Yeye huwapenda sana wanyama na ana mbwa kwa jina Osito ambaye mara kwa mara hupakia picha za video zake kwenye Instagram.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad