Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine yuko mahututi katika Hospitali ya Wilaya ya Longido baada ya kuvuta hewa nzito ya baruti ndani ya mgodi wa madini ya rubi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba tukio hilo lilitokea usiku wa Juni 30.
Alimtaja marehemu kuwa ni Baraka Lenguti (28) mkazi wa KIA wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro ambaye maiti yake ilichukuliwa na askari polisi wa Longido kwa ajili ya uchunguzi.
Alisema kwamba majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Longido hajafahamika na bado yuko mahututi.
Kamanda Ng’anzi alisema mkasa huo umetokea baada ya wachimbaji hao kuingia ndani ya mgodi kabla ya muda wa saa 48 baada ya ulipuaji wa baruti kufanyika.
Alisema kwamba kwa mujibu wa kanuni za madini zilizowekwa na Serikali wachimbaji wakishalipua baruti katika miamba husubiri kwa muda wa saa 48 ndipo wanaruhusiwa kuendelea na shughuli.