Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) jana tarehe 14 Julai, 2018 amekutana na viongozi wa Shirikisho la Muziki, Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho, Shirikisho la Filamu, Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya na Chama cha Muziki wa Dansi na wanasanaa kujadili utekelezaji wa Kanuni mpya za BASATA za mwaka 2018 uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikao kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Katibu Mtendaji wa BASATA na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu.
Kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yaliyomo katika Kanuni hizo pamoja na changamoto zinazowakuta wanasanaa nchini.
Wadau walichangia hoja zao ikiwemo changamoto ya tozo ya kazi za sanaa kwa mtangazo (branding) ya shs. milioni 5 ambayo wamesema itanyima fursa za kupata kazi za matangazo.
Waziri Mwakyembe akijibu hoja hizo alisema Kanuni hizo zilipitia hatua zote ikiwemo kuwashirikisha wadau wote katika hatua za awali na kabla hazijasainiwa.
"Ninayo majina ya wanasanaa walioshirikishwa kwenye vikao vya wadau, hata hivyo wasanii wengi wamekuwa na tabia ya kutoitikia wito na baadaye huja na malalamiko baada ya maamuzi kuwa yameshafanyika", alisema Waziri Mwakyembe.
Kuhusu suala la tozo ya matangazo, Waziri Mwakyembe ameamua kuunda kamati ndogo ya wasanii ambayo itakutana na BASATA kujadili njia mbadala ya tozo hiyo.
Waziri Mwakyembe ameelezea kwamba Kanuni mpya pia zimeongeza muda wa kumbi za muziki zilizo wazi kufungwa saa 6:00 usiku kwa siku za kazi na saa 8:00 usiku kwa wikiendi na siku za sikukuu.
Akijibu kuhusu Utekelezaji wa hoja hiyo ya tozo ya matangazo, Katibu Mtendaji wa BASATA alisema tozo hiyo haizihusu asasi na kampuni za wasanii zilizosajiliwa ambazo zinaweza kujihusisha na matangazo.
Aidha, Katibu Mtendaji wa BASATA ameelezea kwamba tozo ya kumbi za maonyesho pia hiziwahusu wasanii waliosajiliwa na kampuni/asasi wanazozimiliki na kusajiliwa na BASATA.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu amewata wanasanaa kuzingatia taratibu zilizopo wanapoandaa matangazo yao.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisisitiza umuhimu wa Vyama, Mashirikisho na BASATA kuwa utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kujenga mawasiliano bora ambayo yatakuwa ni daraja katika kutatua changamoto zao mapema.