Mwakyembe Awataka wasanii kung’oa mabango yenye picha zao Barabarani
0
July 15, 2018
Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni, Harrison Mwakyembe amesema msanii ana haki ya kuliondoa bango la matangazo yenye picha yake, iwapo limepitiliza muda wa mkataba.
Ameyasema hayo jana Julai 14, alipozungumza na wadau wa Sanaa jijini Dar es Salaam.
Mwakyembe aliyasema hayo baada ya msanii wa muziki, (Kibonge Mwepesi) kudai kwamba kuna baadhi ya watangazaji wanaofanya kazi na wasanii huacha mabango barabarani na kupitiliza muda wa mkataba waliokubaliana.
“Utakuta msanii kaingia mkataba wa mwaka mmoja lakini bango linakaa hata miaka mitatu, huku msanii akiwa hambulii chochote,” alisema
Akilijibu hilo, Waziri Mwakayembe alisema msanii anayefanyiwa hivyo ana haki ya kuwahoji watangazaji hao na ikiwezekana hata kuyaondoa mabango.
"Moja ya sababu ya kuzibana kampuni zinazofanya matangazo na wasanii ni kutokana na kuwanyonya kwa muda mrefu wasanii wetu,” alisema.
Aliongeza: “Hili nimeliona kwa Msanii Mzee Majuto, ambapo yeye kuna moja ya tangazo limekaa miaka mitano barabarani lakini kaambulia Sh5 milioni jambo ambalo halikubaliki.”
Alifafanua kuwa wasanii wanapaswa kuelewa kuwa kanuni za tozo mbalimbali zilizopitishwa hivi karibuni ni katika kuwafanya wafaidike na kazi zao na aliwashangaa wale wanaozipinga.
"Nina uhakika hakuna kampuni kubwa zinashindwa kulipa Sh5 milioni, nashangaa nyie mnavyowatetea wakati wao hata mmoja mpaka sasa hivi hakuna aliyenijia kulalamika," alisema Mwakyembe.
Tags