Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, kata ya Kala wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Eradi Kapyela ametoweka katika na kwenda kusikojulikana baada ya kudaiwa kumpa mimba mwanafunzi wake wa darasa la saba.
Taarifa hiyo ilibainishwa jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani baada ya Mbunge wa Nkasi Kusini, Desderius Mipata kualalamika ndani ya kikao hicho kuwa ameshangazwa na kitendo cha serikali kutomchukulia hatua mwalimu huyo kwa kitendo hicho.
Amesema mimba kwa wanafunzi wilayani humo bado ni tatizo hivyo jitihada za makusudi za mapambano ni lazima ziendelee na kuwa mwalimu huyo ni lazima achukuliwe hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Missana Kwangulah amesema taarifa za mwalimu huyo wanazo na juhudi za kumsaka zinaendelea kwani muda wa siku tano umepita tangu mwalimu huyo atoweke katika kituo chake cha kazi bila taarifa na kwaamba amefanya hivyo kukwepa mkono wa sheria.