Mwanamitindo Sylvester Afikishwa Mahakamani kwa kukutwa na Madawa ya Kulevya
0
July 28, 2018
Mwanamitindo wa mavazi, Wolfgang Sylvester (25) amefikishwa katika Mahakama ya Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kusafirisha Dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride Kg. 2.49.
Mwanamitindo huyo amesomewa kosa na Wakili wa serikali Janeth Mogolo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega ambapo amedai amekamatwa na dawa hizo July 22, 2018 katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa serikali Mogolo amedai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1)(b) cha sheria ya Dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015.
Mogolo amedai kifungu hicho cha sheria kinaambatana na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya makosa ya uhujumu uchumi kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Wakili Mogolo amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kuisikiliza.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mtega amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo mpaka ipate kibali maalum, hivyo mshtakiwa hapaswi kujibu lolote na mahakama hiyo haiwezi kutoa dhamana.
Hakimu Mtega ameahirishwa kesi hiyo mpaka August 9, 2018 na mshtakiwa amerudishwa rumande.
Tags