Nape Nnauye na Hussein Bashe Wageuka Lulu CCM, Katibu Mkuu Aamua Kutumia Fursa ya Ungangali Wao

Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema wabunge wawili miongoni mwa saba watakaoongoza kampeni za ubunge wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu ni watukutu na wadadisi, ambao CCM inapaswa kujivunia.

Aliwataja wabunge hao kuwa ni Hussein Bashe (Nzega) na Nape Nnauye (Mtama), ambao kwa sasa CCM inapaswa kujivunia kutokana na namna wanavyodadisi mambo na kuyafuatilia, jambo linalofanya mawaziri wafikiri kwa kina kabla ya kutoa majibu na maamuzi.

Dk. Bashiru aliyasema hayo Jumanne ya wiki hii alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM alipopita wilayani Nzega wakati akielekea Kigoma kwenye kampeni za uchaguzi huo zilizozinduliwa jana.

Alisema anamshukuru Bashe kwa kukubali kuwa miongoni mwa wabunge saba watakaoshiriki uzinduzi kampeni hizo katika  Jimbo la Buyungu.

Wabunge wengine watakaoshiriki kwenye kampeni hizo ni Job Lusinde (Mtera), Martha Mlata (Viti Maalumu CCM), Munde Tambwe (Viti Maalumu CCM), Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini), Jackline Ngonyani (Viti Maalum CCM).

“Na kupitia kwenu ningependa kufafanua kuwa Hussein Bashe si mwanachama mkorofi katika chama, lakini ni miongoni mwa wabunge wadadisi, maana kuna tofauti kati ya ukorofi na udadisi na kwa udadisi wake anasababisha tetesi zisizokuwa na ukweli.

“Niwahakikishie, namfahamu kabla hajawa mbunge, Bashe ni mtu mdadisi katika maisha yake niliyomjua mie, ana tofauti kidogo na Nape, Nape kidogo ana joto zaidi kuliko Bashe lakini wote mimi ninawafahamu ni wanachama wadadisi kwa hulka zao.

“Nawafahamu kuwa ni watukutu kweli kweli, wadadisi kwelikweli, lakini wanapishana, kwa kuwa Nape ni mdadisi na mtukutu ambaye joto lake ni kali hivyo kazi yake ni kupooza,” alisema.

Alisema kutokana na udadisi wao na kile ambacho watu wengine wanaona kama ni utukutu, ilifikia wakati baadhi ya wanachama na watu ndani ya CCM walianza kutaka waondolewe, suala ambalo yeye hakubaliani nalo.

Alisema Nape na Bashe ni mfano mzuri wa wabunge wanaochochea usimamizi na kuibua mijadala mizito yenye manufaa kwa Bunge, chama na Serikali.

Dk. Bashiru alisema wanapoona joto linazidi kazi yao ni kulipunguza, kwa kuwa wanapozungumzia nidhamu hawazungumzii kunyamazisha watu kwa sababu kufanya hivyo kutafanya kukosekane mijadala na fikra mpya.

“Kwa hiyo msikubali kudanganywa kwamba Bashe na Nape ni watukutu, si watukutu, ni wadadisi kwa hiyo ninawashukuru sana kumchagua Bashe maana anachangamsha Bunge na anawafanya mawaziri wa CCM kufikiri kabla ya kutenda.

“Maana kutenda kila mmoja anaweza kutenda, hata mwendawazimu anaweza kutenda lakini ili utende kwa ufanisi na tija unahitaji kufikiri na kwa hiyi michango yake katika Bunge inawafanya mawaziri wafikiri,” alisema.

Alisema mahudhurio ya Bashe na Nape bungeni ni mazuri na kuwapa alama ya A na kwamba amepitia mahudhurio na kuona wapo wabunge wasiohudhuria bungeni na wengine hawajawahi kuwasikia hata mara moja wakichangia.

Alisema ameanza kuchambua mahudhurio hayo tangu kuanza kwa Bunge hadi siku ya bajeti na kubaini kuwa baadhi ya wabunge walihudhuria kikao kimoja tu kati ya 15 vya wabunge wa CCM (part caucus).

“Tena waliingia katika vikao vilivyokuwa vinahusu agenda inayowahusu,” alisema.

Alisema watatumia kanuni kuwaadabisha hadi watakaposhika adabu na kuwataka wabunge watambue kwamba ubunge ni mali ya wananchi kupitia chama kilichowadhamini.

Dk. Bashiru alisema kwa kuwa hakuna utaratibu wa wapiga kura kuwawajibisha wabunge kabla ya muda, watashughulikiwa ndani ya chama.

Alisema shabaha ya tatu ya Ilani ya CCM ni kupambana na rushwa na ufisadi bila woga kwa rais aliye madarakani na katibu mkuu wa chama kutokuwa wala rushwa ili mashambulizi yaanzie Ikulu na makao makuu ya chama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad