Nyimbo za Siku Hizi ni Bigijii- Master J

Nyimbo za Siku Hizi ni Bigijii- Master J
Muandaaji wa muziki nchini, Master J ameweka wazi kuwa anasikitishwa na baadhi ya wasanii kupenda kutengeneza kiki katika utoaji wa nyimbo zao na kupelekea kupoteza mvuto kwa wasikilizaji muda mfupi baada ya kutolewa na kuziona kama 'bigijii' ambazo hutafunwa kwa muda mfupi na kuisha utamu

Akizungumza na www.eatv.tv, Master J ameeleza kuwa chanzo cha yeye kulalamika juu ya wasanii hao  ni kwa sababu mtindo huo hauendelezi bali unaua muziki wa Tanzania, na kuongeza kuwa ni wazi jambo hilo limeshamiri kwa kiasi ambacho mara nyingine aonapo fujo za baadhi ya wasanii katika mitandao, yeye huwaelewa moja kwa moja kuwa wanampango wa kutoa wimbo.

"Hakuna kitu kinachoua muziki dunia nzima kama kiki, lakini ndiyo tulipo huko kwa sasa. Hili ni tatizo, na sio kwetu tu hata nchi za nje kama Marekani na Nigeria lipo. Licha ya kuwa hapo ndipo wasanii wanapotengenezea pesa zao, ila mwisho wake tutaujua tu. Mimi nalalamika sababu navyoona tunapoelekea siyo pazuri, sisi tulifanya kazi kubwa sana kujenga misingi ya muziki wetu", amesema Master J.

Pamoja na hayo, Master J ameendelea kwa kusema "haiwezekani mpaka mtu akae nusu utupu ndiyo iwe kiki ya kutoa wimbo wake. Mfano wiki hii nimeshaona wasanii wakubwa wakifanya fujo kwenye mitandao ya kijamii nikajua hawa wanataka kutoa wimbo, na cha ajabu wametoa kweli wimbo kupitia fujo zao mitandaoni".

Hata hivyo Master J ameeleza utofauti wa muziki uliokuwa unafanywa enzi za zamani kuwa ulikua na maudhui, yaani nyimbo ambazo mtu alikuwa na uwezo wa kuchambua mfano zile zilizokuwa zikiongelea masuala mbalimbali yanayoikumba jamii. Tofauti na baadhi ya muziki wa kileo ambapo hukosa maudhui hayo.

"Mfumo wa muziki umebadilika , zamani tulikua tukitengeneza muziki wenye maudhui tofauti na siku hizi mfano Muheshimiwa Sugu enzi hizo unaweza ukachambua baadhi ya nyimbo zake zikizungumzia vitu ambavyo vipo kabisa kwenye jamii mfano unyanyasaji wa raia unaofanywa na polisi, unyanyasaji wa wanawake na mengineyo. Yani kifupi ilihitaji ubunifu wakuzungumzia mambo huku ukiburudisha....

Wasanii wa siku hizi wanafanya muziki kama bigijii ambayo ukiweka mdomoni utatafuna na baada ya muda inaisha utamu, hivyo mtu akisikiliza atachoka tuu. Na sio tu wasanii watanzania wanafanya hivyo bali hata wamarekani na wanigeria. Kipindi hiko unakuta wasanii kama Ray C, Mr Paul, Juma Nature na wengineo hata wasipotoa wimbo mwaka mzima bado wakirudi ngoma huendelea na kasi ya utamu ule ule", amesisitiza Master J.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad