Pacha wa Tanzania waliozaliwa wakiwa wameungana kifuani hadi miguuni mkoani Kagera mapema mwaka huu wamewasili nchini Saudi Arabia kwa upasuaji wa kuwatenganisha.
Anisia na Maryness Beautus waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh wakiandamana na mama yao na kundi la madaktari.
Kisa cha pacha hao kimefananishwa na kisa cha pacha wengine walioungana waliogusa nyoyo za wengi nchini Tanzania Maria na Consolata. Hao hata hivyo hawakutenganishwa na waliishi wakiwa wameungana hadi walipofariki dunia tarehe 2 Juni mwaka huu.
Pacha hao Anisia na Maryness watafanyiwa upasuaji karibuni baada ya Mfalme Salman kutoa idhini ya kufanyika kwa upasuaji huo kwa gharama ya serikali ya Saudia.
Pacha hao walipokelewa na kikosi maalum cha wanajeshi walinzi wa rais na maeneo matakatifu ya Kiislamu katika uwanja wa ndege. Wanajeshi hao walisaidiana na wataalamu kutoka Kituo cha Misaada ya Mfalme Salman (KSRelief) ambao watasimamia matibabu yao na kuchunguza iwapo inawezekana kuwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha.
Pacha hao wawili wenye miezi sita wameungana kutoka kwenye koo, tumbo na mfupa wa nyonga. Wana miguu mitatu na kwenye uzazi. Hata hivyo, kila mmoja ana moyo wake.
Wamekuwa wakihudumiwa na madaktari katika hospitali ya taifa ya Muhimbili nchini Tanzania na wamekuwa katika hali nzuri.
Mfalme Salman alitoa agizo la kufanikishwa kwa matibabu ya pacha hao Jumapili ambapo aliagiza pia kwamba Saudi Arabia ilipie gharama yote ya upasuaji huo.
Ujumbe kutoka kwa ubalozi wa Saudia nchini Tanzania ulikuwa umewatembelea pacha hao Muhimbili, Dar es Salaam awali na kupokea taarifa za kimatibabu kuwahusu pacha hao kutoka kwa mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt Lawrence Museru.
Pacha hao wa Tanzania walizaliwa mnamo 29 Januari mwaka huu katika zahanati ya St Thereza Omukajunguti wilayani Misenyi. Walisafirishwa hadi hospitali ya kanda ya Bukoba kabla ya mwishowe kuhamishiwa Muhimbili.
Baba yao Benatus Bernado, 28, alikuwa awali ameambia gazeti la serikali ya Daily News kwamba waikuwa wameshauriwa na madaktari Muhimbili kwamba wataalamu wa Saudi Arabia ndio waliokuwa na uwezo wa kuwatenganisha pacha hao.
Serikali ya tanzana imekuwa ikifanya mashauriano ya kufanikisha kuhamishiwa kwa pacha hao Tanzania kwa wiki kadha, mazungumzo yaliyomshirikisha balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mohammed Bin Mansour Almalik na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Dkt Augustine Mahiga.
Pacha Walioungana Wawasili Saudi Arabia kwaajili ya Kutenganishwa
0
July 10, 2018
Tags