Peter ndiye Baba Shujaa wa Patrick, Siyo Aliyekimbia Mimba. Wanaume Aina ya Peter ni Wachache


From @luqmanmaloto - DOOH MUNA! TUACHE TU PATRICK APUMZIKE

KUNA mwanamuziki wa Bongo Fleva mkubwa, naye alipatikana mfano wa mtoto Patrick kama alivyosimulia Muna. Mama yake akiwa mjamzito, alikutana na mwanaume ambaye alikubali kubeba majukumu ya mume na kuwa baba wa mtoto tumboni.

Mtoto alizaliwa. Yule mwanaume akawa baba rasmi. Cheti cha kuzaliwa kikaandikwa jina la yule mwanaume. Hata shule aliandikishwa kwa ubini huo. Mpaka leo, mwanamuziki huyo hamfahamu baba mwingine, isipokuwa huyo mwanaume aliyempokea mama yake na ujauzito.

Muna amesimulia kuwa alikutana na Peter Kosovo akiwa na ujauzito wa wiki mbili. Peter akamuoa Muna na mimba yake. Muna anasema, Casto Dickson ndiye baba wa mtoto, lakini aliikataa mimba. Peter akamchukua Patrick kama mwanaye kabisa. Hivyo, Patrick alizaliwa na kujikuta ana mama na baba rasmi ambaye ni Peter.

Thamani kubwa ya Peter ipo kwa Patrick. Mtoto anapozaliwa na kuona mama na baba yake wapo pamoja, humjenga kujiamini na kujiona amezaliwa katika mfumo rasmi. Hivyo, ilikuwa wajibu wa Muna na Peter kuendelea kubaki wazazi wawili wa Patrick bila kumvuruga.

Kitendo cha Peter kumng'ang'ania Patrick kina maana ya kumlinda mtoto asivurugwe kisaikolojia. Mtoto anafikisha miaka mitatu ndiyo anaambiwa baba mwingine aliyemkimbia akiwa mimba, aliyempokea na kumjua mpaka alipofikisha umri huo eti anakuwa si baba tena.

Kama yule mama wa mwanamuziki mkubwa wa Bongo Fleva na Muna, ndani ya familia nyingi hutokea. Baba na mama hukubaliana iwe siri yao chini ya falsafa ya "Kitanda hakizai haramu." Mtoto hukuzwa bila kuona tofauti yoyote kwa wazazi wake. Tatizo Peter alikosea mwanamke wa kutunza naye siri. Muna alistiriwa, yeye kajivua stara yote.7

Labda alidhani anamuumbua Peter, ila alijiumbua yeye na kumuumiza mtoto. Pengine Patrick katika ukubwa wake Mungu angemuweka hai, angemsema sana Muna na sinema zake zenye utoto mwingi kiasi cha kumdhalilisha. Thamani ya mtoto ni baba mmoja.

Peter ndiye baba shujaa wa Patrick. Siyo Casto aliyekimbia mimba. Wanaume aina ya Peter ni wachache. Hawazaliwi kila siku!

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad