Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakina wasiwasi wa aina yoyote na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika uchaguzi mdogo wa marudio wa Ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma huku kikidai waoitilia shaka tume hiyo wao ndio wenye matatizo.
Hayo yamelezwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole wakati akizungumza na www.eatv.tv baada ya kupita takribani siku tatu tokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoa kauli yake iliyokuwa ikiitaka NEC kuendesha uchaguzi huo kwa uhuru na haki kuwa kuna baadhi ya vitu wamevibaini vikiendeshwa ndivyo sivyo.
"Sisi hatuna mashaka yoyote na Tume ya Uchaguzi (NEC) na kama tungekuwa nayo basi tungeshayaeleza mahali husika ila ukiona mtu anajitokeza barabarani na kusema kuna changamoto bila ya kuzipeleka sehemu husika basi ujue yeye ndiyo mwenye changamoto nasio Tume", amesema Polepole.
Pamoja na hayo, Polepole ameendelea kwa kusema "Chama cha Mapinduzi kimejiwekea rekodi ya kushughulika na shida za watu na kutatua kero za wananchi wa Tanzania na hili limefanyika vizuri sana chini ya serikali ya CCM inayoongozwa na ndugu John Magufuli. Tumekuwa hatuna mzaha, masihara na watu wanaocheza na rasilimali za umma, wanaonyanyasa wananchi, wasiowajibika na kushughulika na shida za watu na kwa rekodi ambayo tumeshajiwekea mpaka sasa hivi tutaenda kupanda ushindi mkubwa wa kishindo kwasababu ya kazi ile nzuri ambayo tumekwisha ifanya hadi sasa hivi".
Uchaguzi huo mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Agosti 12 mwaka huuu baada ya kuwepo wazi Jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma kufuatia Mbunge Kasuku Bilago kufariki dunia mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu pamoja na madiwani wa maeneo mbalimbali kuyaacha majimbo yao na kujiunga CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli.