Rais Ateua, Waziri Avunja Uteuzi
0
July 24, 2018
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Kazi Vijana na Ajira Jenista Mhagama ameivunja bodi ya wadhamini ya Shirika la Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kile alichodai ni kuimarisha shirika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Jenista ametangaza kutengua uteuzi wa wajumbe wote wa bodi, wakati Akizungumza na wanahabari leo Julai 24 2018, jijini Dodoma ambapo amesema kuwa utaratibu wa uteuzi wa bodi mpya unafanyika.
"Kwa mujibu wa aya ya 2(1)(A) ya jedwali la Sheria ya NSSF Rais ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, hivyo ameridhia kutenguliwa kwa uteuzi wa Mwenyekiti wa sasa wa bodi hiyo kuanzia leo," amesema Jenista.
Amesema lengo mabadiliko haya ni kuhakikisha kuwa shirika linamarishwa zaidi katika kusimamia mwenendo wa kila siku wa shirika ikiwamo kazi ya msingi ya kuongeza wanachama kukusanya michango, kulipa mafao kwa wakati na kusimamia vitega uchumi kwa uzalendo.
Utenguaji huo unakuwa ni mwendelezo wa Waziri Jenista ambaye Julai 17, 2018 alitangaza kutengua uteuzi wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TaESA), Saneslaus Chandarua huku akitaja sababu za kumtengua mkurugenzi huyo kuwa ni pamoja na kushindwa kuunganisha watafuta kazi na waajiri, kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa ajira ndani na nje ya nchi, kukusanya, kufanya uchambuzi na kusambaza taarifa za soko la ajira kwa wadau na umma kwa ujumla.
Tags