Rais John Pombe Magufuli leo amekabidhi hati za kumiliki viwanja makao makuu ya nchi Dododma kwa Mabalozi wa nchi mbalimbali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ikiwa ni azma ya serikali yake kuhamia Dodoma kabla ya mwaka huu kuisha.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hati hizo Rais Magufuli amesema serikali ya awamu ya tano imeamua kutekeleza kwa vitendo maneno mazuri ya hayari Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamia Dodoma, hivyo ameona sio vema yeye kuhamia Dodoma na kuwaacha mabalozi na wawakilisha wa marais wa mataifa mbalimbali jijini Dar- esa Salaam na ndio maana ameamua kutoa hati hizo mapema.
Rais Magufuli amesema serikali imeamua kutoa bure maeneo yenye ukubwa wa zaidi hekari tano kwa ajili ya Mabalozi na taasisi mbalimbali lengo likiwa ni kuonesha urafiki uliopo wa mataifa na nchi zinazowakilishwa na viongozi hao, na kwamba viongozi mbalimbali wa serikali yake tayari wamekwisha hamia Dodoma ikiwa ni pamoja na watumishi karibu 60,000.
Amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme, huduma za jamii hasa afya, elimu, maji na usafiri ambapo mkoa wa Dodoma umeunganishwa na barabara za lami na mikoa yote inayozunguka yani Morogoro, Singida, Manyara na Iringa.
Ameongeza “Leo nimetoa maagizo kwa Viongozi wa TANROADS watangaze tenda kwa ajili ya kuanza ujenzi mkubwa wa uwanja wa Msalato ili ndege kubwa zinazotua Dar- esa Salaam zitue Dodoma nimefurahi kumuona mwakilishi wa African Development Bank ( Banki ya Maendeleo ya Afrika) tulizungumza na rais wa benki hiyo kwamba watatoa dola milioni 200 tumeshawaandikia barua ninauhakika watazitoa mapema kwa sababu tumewapa hati ya bure ya kukaa Dodoma”.
Rais Magufuli ameeleza kuwa wakati serikali ikisubiri fedha hizo kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika ametoa maagizo ya tenda kutangazwa ili kazi ya ujenzi wa uwanja huo mkubwa wenye urefu wa zaidi ya kilimeta 3 ianze mara moja ambapo ndege ya aina yoyote inaweza kutua ikiwamo ndege mpya ya serikali Boeing Dreamliner 787-8 pamoja na ndege nyingine kubwa kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi, Mashirika na Wawakilishi hao wa Mataifa mbalimbali waliopokea hati hizo kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa ya ukubwa wa viwanja walivyopewa kwa kuwekeza ipasavyo hasa kwa kujenga majengo ya ubalozi, sehemu za biashara na makazi kuliko kuendelea kubanana jijini Dar- es Salaam.