Kwa jinsi teknolojia inavyokuwa kwa kasi duniani hakuna ubishi kuwa mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa sana hii sio tu kwa ajili ya kupata habari kwa wakati bali kusaidia viongozi pia kutoa taarifa kwa wakati pale kunapotokea tatizo.
Sasa kwa bahati mbaya kumekuwa na wahuni ambao wamekuwa wakidukua kurasa za watu maarufu na viongozi na hili limewatokea Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
RC Makonda yeye akaunti yake ya Instagram ambayo ilikuwa na wafuasi zaidi ya Milioni Moja imepotea ghafla toka jana haionekani mtandaoni.
Watu wa karibu na RC Makonda akiwemo Babu Tale alitoa taarifa hizo jana kwa kuandika “Watu waliokosa uoga wameondoka na account ya mkuu wa mkoa wa Dar leo Mhe. Makonda @paulmakonda”
Wakati hayo yakijiri nchini Kenya nako akaunti ya Twitter ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ya (@PresidentKE) nayo imepatwa na majanga kwa kupotea ghafla mtandaoni.
Hata hivyo, kesi ya ukurasa huo kupotea ni tofauti kidogo na ya RC Makonda kwani ukurasa wa @PresidentKE umefutwa kabisa na Twitter wenyewe kwa kukiuka masharti.